SHIKAMOO Wema! Shikamoo dada Wema! Ndiyo iliyokuwa salamu na topiki kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita.
Ilikuwa ni baada ya wewe mwigizaji kinara wa filamu za nyumbani, Wema Isaac Sepetu kumnusuru staa mwenzako, Kajala Masanja.
Kweli ulimuokoa kwenda jela miaka saba kwa kumlipia faini ya Sh. milioni 13 za madafu.
Kama ulikosa muda wa kupitia maoni katika mitandao ya kijamii,
nitakwambia. Maoni yalikuwa mengi hasa yale ya kukusifia. Wengine
walikuita dada, wengine mama pamoja na kwamba wamekupita kiumri.
Kweli Wema umelitendea haki jina lako kwa kutenda wema kwa wengine japo
leo nitakupa matukio yako ya kufuru katika kipindi kifupi kisichozidi
miezi kumi. Kufuru zote ulianza Juni, mwaka jana na tayari umeteketeza
zaidi ya Sh. milioni 800 katika ghughuli zako. Nitaziorodhesha ‘then’
tutajadili walau kidogo kwa kuwa wewe ni mmoja wa vijana watafutaji.
Kuhusu kufuru zako sishangai kwa kuwa zinahamasisha vijana kutafuta
mkwanja. Kama wewe ni mfuatiliaji wa soka la England nitakwambia kitu.
Unakumbuka tukio la kufuru ya fedha la aliyekuwa straika wa Manchester
City ya England, Mario Balotelli kabla ya kutua AC Milan? Siku moja
alinaswa kule England akitapanya Sh. milioni 100 akakamatwa na
kufunguliwa mashitaka. Wewe umeona usifanye kama Balotelli. Unafanya
yako!
Katika kipindi hicho cha miezi kadhaa umefanya mambo makubwa. Nawatazama matajiri wa Kibongo sioni mwenye makeke kama yako.
Nitakukumbusha! Katikati ya mwaka jana ulitamba kununua nyumba
Kijitonyama, Dar kwa Sh. milioni 400. Haikutosha ukaikarabati na kuweka
samani kwa Sh. milioni 30.
Wakati wadadisi wa mambo wakimwaga data
kuwa ni jeuri ya fedha za mume wa mtu, wewe uliziba masikio, ukazama
Dubai ukawaziba midomo kwa shopping ya Sh. milioni 60.
Nakumbuka
ulizindua filamu yako ya The Super Star kwa kumleta staa mkubwa wa
Nollywood, Nigeria. Gharama zote zilikuwa ni Sh. milioni 40 na kufuatiwa
na makeke mengine ya ununuzi wa magari ya bei mbaya. Ulinunua Toyota
Lexus Harrier, Sh. milioni 25, Toyota Mark X, Sh. milioni 60 na Audi Q7
la Sh. milioni 80.
Weka mikoko pembeni, uzinduzi wa ofisi yako ya
Endless Fame ulikuwa gumzo, taarifa zilieleza kuwa ulitumia zaidi ya Sh.
milioni 70. Mengine ni kufuru ya kuwafanyia mbwa wako shopping ya zaidi
ya Sh. milioni 6, kumwokoa Kajala asiende jela kwa kumlipia faini ya
Sh. milioni 13 na kutunza wasanii wa muziki stejini.
Wema
umeendeleza pale mwigizaji Jacqueline Wolper alipoishia. Wewe umemwokoa
Kajala, yeye alipigania uhai wa mwigizaji Juma Kilowoko ‘Sajuki’ kwa
kumchangia Sh. milioni 16 za matibabu.
Niliwahi kusema hapa kuwa
baadhi ya wasanii wetu hawana kasumba ya kujitolea katika jamii.
Alichokifanya Wema ni cha kupongezwa lakini sasa tunahitaji wajitokeze
wasanii wengine wa kuwasaidia wenzao kama mchekeshaji Said Ngamba ‘Mzee
Small’ anayesumbuliwa na ‘stroke’. Yumo pia mwigizaji Juma Salim ‘Mzee
Kankaa’ anaumwa baada ya kupata ‘stroke’. Bila kumsahau mwingizaji
Ramadhan Mwinshehe ‘Mashaka’ naye kapooza hivyo anahitaji msaada. Ili
kujenga jamii yenye kushikamana, si vyema ikajengeka picha kuwa
wanaostahili kusaidiwa ni wale wa aina fulanifulani bali ifahamike kuwa
kutoa ni moyo na si utajiri. For the love of game!
No comments :
Post a Comment