Top News

Saturday, April 20, 2013

BUNGE LAWANUSURU USALAMA WA TAIFA WANAOTAJWA KUHUSIKA NA UTEKAJI

Bunge limekataa kuamuru Serikali kuchukua hatua dhidi ya tuhuma dhidi ya baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa wanaodaiwa kujihusisha kuteka na kutesa watu.
Bunge limefikia uamuzi huo juzi kwa kupiga kura za sauti, kupinga hoja ya Msemaji wa Kambi wa Upinzani katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Profesa Kulikoyela Kahigi.
Profesa Kahigi alitaka Bunge liitake Serikali kuchunguza tuhuma hizo na kuwachukulia hatua watuhumiwa hao, suala ambalo liliibua mvutano baina ya Kambi ya CCM na Serikali kwa upande mmoja na upinzani kwa upande mwingine.
Mvutano huo ulitokea juzi wakati Bunge limekaa kama kamati kupitisha kifungu cha mshahara wa Waziri.
Profesa Kahigi alisema kambi yake imetoa tuhuma dhidi ya maofisa usalama wa taifa, kuwatesa watu na kutumika kupanga njama, lakini Serikali imekaa kimya bila kuchukua hatua dhidi ya tuhuma hizo.
“Ninachoomba ni kitu kidogo tu, hoja yangu hapa ni kwa nini Bunge na Serikali havichukui hatua, ninatoa shilingi mpaka mtakapoeleza ni hatua gani mtazichukua dhidi ya tuhuma hizi,” alisema Profesa Kahigi.
Suala hilo lilizua mjadala na kusababisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kusema Bunge siyo sehemu ya mashtaka na kwamba, kama kambi hiyo inazijua tuhuma hizo izipeleke polisi huko ndiyo hatua zitachukuliwa.
“Nendeni polisi mpatiwe RB (Kumbukumbu ya taarifa polisi) halafu tuhuma zitafuatiliwa. Hatuwezi kwenda kuwashughulikia hao watu mnaowasema,” alisema.
Chikawe.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema tuhuma hizo kisheria zinatakiwa zipelekwe polisi siyo bungeni.
“Hatuwezi tukashughulikia tuhuma kwa kuwa tu mmesema kwamba tuzichukulie hatua,.Naomba wanasheria wenzangu tufuate sheria kwa kuwa tunazijua,” alisema Simbachawene.
Hata hivyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alipinga hilo na kwamba, kazi ya Serikali ni kuchukua hatua dhidi ya tuhuma zinazotolewa bungeni na mahali pengine siyo kuzungukazunguka.

No comments :

Post a Comment

Designed By ApexbnewZ