Top News

Friday, May 3, 2013

LISU ATEMA CHECHE: AFICHUA MAWASILINO YA SIRI YA CCM YA UCHAKACHUZI WA MCHAKATO WA KATIBA SOMA HAPA

Barua pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro inasema: “Naandika kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa Makatibu wa Mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba. Kama mnavyofahamu Tume ya Katiba imeshatoa taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari ... kuhusu zoezi hili muhimu. Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, hivi sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea.”

Baada ya kuagiza ‘mawasiliano kati ya SUKI na Makatibu wa Mikoa’ kuhusu mambo ya kufanya, Dr. Asha-Rose Migiro alimalizia barua yake kwa maneno yafuatayo: “Tafadhali wanakaliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.” ‘Wanakiliwa’ wa barua pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro ni pamoja na Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakhia Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib na Bw. Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa NEC ya CCM.

Siku moja baadaye, Nape Nnauye aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake kama ifuatavyo: “NASHAURI ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa swala hili tupate taarifa kila siku/au walau siku tatu ya HALI HALISI inavyoendelea katika kila mkoa, ni vizuri idara ikaandaa checklist ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la! Mfano ... idadi ya walioandaliwa kugombea katika kila eneo, idadi ya waliohamasishwa kuhudhuria na kupiga kura, n.k.”

Mnamo tarehe 18 Desemba mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Francis K. Mwonga, aliwaandikia barua Makatibu wote wa CCM wa Mikoa kuwapa ‘Maelekezo ya Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Makatibu wa CCM wa Mikoa Kilichofanyika Dar es Salaam Tarehe 10/12/2012.’

Sehemu ya Maelekezo hayo inasema: “Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi.” Maneno haya yameandikwa hata kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi na tayari Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ juu ya namna ya kupanga vituo vya kupigia kura.

 Mawasiliano haya ya viongozi wa ngazi za juu za CCM yanathibitisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya umeiingiliwa na kuhujumiwa kwa kiasi kikubwa na CCM. Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli iliyotolewa mbele ya Bunge lako tukufu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba “...viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kwamba wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika chaguzi za vijiji, mitaa au kata.” Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyochaguliwa kwa utaratibu “...ni mabaraza ya CCM na sio mabaraza ya katiba ya Watanzania wote.”

1 comment :

  1. hawa watu hawana lengo zuri na Taifa.kama wananchi wasipokua makini Taifa linakwenda kuangukia mikononi mwa kundi la watu wachache wasio na uzalendo kwa nchi yao.Hata hivo hakuna lisilo na mwisho pamoja na mbinu zao zote watu wamefunguka na hawatafanikiwa.

    ReplyDelete

Designed By ApexbnewZ