Hakuna barabara kwangu, kwa nini niunge mkono hoja?
Namshangaa sana Kapuya kwa tabia aliyonionyesha pale... Mbona mama
Margaret Sitta amesema Tabora hakuna barabara hawakumfuata
Wabunge
wa CCM, jana walizua tafrani nje ya Ukumbi wa Bunge baada ya
kukasirishwa na kitendo cha mwenzao wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy
kupinga Bajeti ya Wizara ya Ujenzi wakati akichangia hotuba ya wizara
hiyo.
Katika mchango wake, Keisy alisema haungi mkono hoja kwa sababu Barabara
ya Sumbawanga hadi Kanazi-Mpanda mpaka Kibaoni haijajengwa kwa kiwango
cha lami.
Alisema zilitengwa Sh27 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo
lakini mpaka sasa Wachina waliopewa zabuni ya ujenzi huo wamekosa fedha
na wameamua kuuza kokoto.
Mara baada ya Bunge kuahirishwa, Keisy akiwa nje ya ukumbi huo alifuatwa
na Mbunge wa Urambo Mashariki, Profesa Juma Kapuya, Omary Nundu (Tanga
Mjini), Mendrady Kigola (Mufindi Kusini) na Rita Kabati (Viti Maalumu)
na kumzonga.
Baada ya wabunge hao kumzonga, Profesa Kapuya ambaye amewahi kuwa waziri
serikalini alihoji kitendo cha mbunge huyo kupinga bajeti... “Kwa nini
umekataa kuunga mkono hoja? Ulikuwa unalidanganya Bunge wakati
unachangia si kweli huko Rukwa hakuna barabara, barabara mnazo.”
Kessy alionekana kukerwa na swali hilo na kumjibu kwa hasira: “Nyinyi na
mimi nani ni mbunge Nkasi? Mimi sina unafiki napinga kutokana na
yaliyopo jimboni kwangu sipo hapa bungeni kuwafurahisha nyinyi na wala
Serikali. Nipo kwa masilahi ya wananchi wangu.” Baada ya majibu hayo,
mbunge huyo aliondoka haraka eneo hilo.
Baadaye jioni mwandishi wetu alimfuata ili kupata ufafanuzi juu ya
msimamo wake... “Hakuna barabara kwangu, kwa nini niunge mkono hoja?
Namshangaa sana Kapuya kwa tabia aliyonionyesha pale... Mbona mama
Margaret Sitta amesema Tabora hakuna barabara hawakumfuata?”
Alisema wabunge hao hawana haki ya kuhoji kwa nini hakuunga mkono hoja
kwa kuwa kila mmoja amekuja bungeni kutokana na kushinda katika jimbo
lake. Akichangia hotuba ya bajeti hiyo, Kessy alisema haungi mkono hoja
kwa asilimia 100 hadi pale atakapoelezwa lini barabara hizo zitajengwa.
Alisema zaidi ya vijiji 30 vya mwambao wa Ziwa Tanganyika na Barabara ya
Kipili hadi Bandarini ni mbovu kwa kiasi kikubwa na muda wake wa ujenzi
kumalizika umeshapitiliza miezi mitatu iliyopangwa.
Alisema nchi imegawanyika kwani baadhi ya majimbo ya wabunge yana lami
hadi mlangoni lakini Nkasi hawajawahi kuiona akitoa mfano wa Jimbo la
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (Mpanda Mashariki) Same Mashariki kwa Anna Kilango.
No comments :
Post a Comment