BINTI aitwaye Nuru Omari anayedaiwa kufariki dunia mwaka 2010 ameibuliwa
hivi karibuni wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani na mganga akiwa hai
kwenye banda kuukuu.
Binti Nuru Omari aliyeibuliwa.
Tukio hilo limetokea kwenye Kijiji cha Kalole, Tarafa ya Kisiju, walayani humo.
Kwa mujibu wa baba wa binti huyo, Omari Salum, mwaka 2010 ndugu wa mkewe
aitwaye Nyasenene aliyekuwa akiishi Charambe Mbagala, jijini Dar
alifika nyumbani kwake na kuwaomba wampe mtoto wao kwa ajili ya kwenda
kufanya kazi za ndani ‘hausigeli’.
Kijumba alimokuwa Nuru.
Baada ya binti huyo kufanya kazi kwa muda mfupi aliugua malaria, baba
mtu akapewa taarifa na kufika Dar kwa ajili ya kumuona mwanaye
aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar.
Mzee huyo amesema alikwenda Muhimbili na kufanikiwa kuzungumza machache
na mwanaye huyo ambapo alikuwa akilalamikia maumivu ya tumbo.
Ndugu na majirani waliofika kumtazama Nuru.
Mzee huyo alisema ilibidi aondoke licha ya mwanaye kumtaka alale lakini
kwa vile yeye ni mwanaume isingewezekana kulala hospitalini hapo.
“Kesho yake nilipewa taarifa kuwa
mwanangu amefariki dunia usiku. Tulianza taratibu za mazishi na kumzika
kwenye Makaburi ya Kichangani, Mbagala, Dar kutokana na kukosa fedha za
kuusafirisha mwili hadi Mkuranga,” alisema mzazi huyo
Mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Said Ali Ngaora ‘Dr. Lamba’
anayeishi Mbagala Rangi Tatu, Dar alifika katika kijiji hicho cha
Kalole mwaka huu na kuwaambia wananchi kuwa kijijini hapo pana mtu
anaonekana alikufa na kuzikwa lakini bado yupo hai na amewekwa sehemu na
kutaja gharama za kumtoa ni shilingi milioni tatu.
Mganga aliyemuibua Nuru.
Akielezea tukio zima Dr. Lamba alisema wananchi walimruhusu akaanza kazi kwa kushirikiana na wataalamu wenzake.
Dr. Lamba na timu yake walifanikiwa kumuibua msichana huyo anayekadiriwa
kuwa na miaka 12-15 kwenye mji ambao hakuna mtu anayeishi akiwa ndani
ya banda la kuku huku kukiwa na chungu chenye damu, asali na udongo
ambavyo vilikuwa ndivyo vyakula vyake akiwa na muonekano wa kutisha kwa
kuwa na nywele ndefu na chafu na kucha zikiwa ndefu mithili ya jini.
Baada ya kumtoa alipelekwa katika uwanja wa mpira kijijini hapo na
kuogeshwa pamoja na kukatwa kucha kisha akapelekwa katika nyumba
aliyofikia mganga huyo, hata hivyo hakuweza kuongea vizuri.
Kwa mujibu wa mashuhuda ulimi wa Nuru ulikuwa mzito na mpaka sasa
anazungumza kwa vitendo kama bubu huku chakula ambacho ameanza kula
vikiwa ni ugali na kuku, uji na juisi ya embe.
Mbali na shilingi milioni tatu za kutoa, mganga huyo anataka milioni 15
kutokana na dawa anazompa kwa ajili ya matibabu ili arudi katika hali
ya kibinadamu .
Hata hivyo, baadhi ya ndugu wanaopinga kuwa Nuru siyo mtoto wao lakini
baba mzazi anasema ni mwanaye kutokana na alama zilizopo mgongoni mwake
na anafanana sana na mdogo wake.
Makamu Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ali Hassan Ndeko alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka sasa wanakijiji wanaendelea
kumiminika kwa ajili ya kumuona mtoto huyo akiwa chini ya uangalizi
maalumu wa mganga huyo huku wakijitolea vyakula.
No comments :
Post a Comment