Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) amekanusha
kutoroka hospitalini jijini Arusha na badala yake ameshukuru Naibu
Waziri na Mbunge kwa kumhangaikia.
Akizungumza jana katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa
baada ya kuhamishiwa hapo kutoka Arusha, Mbunge huyo alisema alipewa
rufaa na huduma ya kusafirishwa kwa ndege hadi MOI.
Alimshukuru Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi) kwa
jitihada za kuhangaika pamoja na Ofisi ya Bunge na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kukodi ndege iliyomwezesha kufika
hospitalini MOI.
Nassari alisema hayo wakati akiendelea na vipimo vya shingo na uti wa mgongo hospitalini hapo.
“Nawashukuru sana Nyalandu na Mbatia,
kwani baada ya kusikia ninaumwa na nimelazwa, amekuwa (Mbatia)
akihangaika na kujulisha ofisi za Bunge kuhakikisha ninapewa huduma,
ambapo walikodi ndege na kunifikisha hapa,” alisema Nassari.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema Nassari anaendelea na
vipimo hivyo ambapo jana alitakiwa kufanyiwa kipimo cha MRI kwa ajili ya
uti wa mgongo na shingo.
Nassari alisimulia, kwamba aliumizwa zaidi
kifuani, kichwani na katika uti wa mgongo, kwani alipigwa sana kwa
marungu jambo lililosababisha kutokwa na damu nyingi puani.
Alisema baada ya kufika MOI, alifanyiwa vipimo kikiwamo cha X-ray na
kuangalia pingili za mgongo na kukutwa ziko sawa ingawa misuli
inayozunguka uti haiko sawa, hivyo kushauriwa kufanya kipimo cha MRI.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa
Ubungo, jana alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema Nassari alitoroka kwenye Hospitali ya Rufaa ya Selian, Arusha ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Mnyika alidai, kwamba Mbunge huyo, alifanya hivyo baada ya kupata hofu
ya kudhuriwa na maofisa wa usalama aliodai walikuwa wamevalia mavazi ya
kidaktari.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mnyika alidai Nassari aliwafahamu
maofisa hao kwa majina, ambao walikuwa wakimtafuta wodini bila kufahamu
walikuwa na lengo gani.
“Baada ya mbunge wetu kubaini hali
hiyo, alipiga yowe ambayo iliamsha wagonjwa waliokuwa wodini na maofisa
hao kukimbia na yeye kutumia fursa hiyo kutoroka ili kuokoa maisha
yake,” alikaririwa Mnyika.
Hata hivyo, Mganga Msaidizi wa Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga
alikaririwa akikanusha taarifa ya Mnyika kwa kusema Nassari alipewa
ruhusa baada ya hali yake kuridhisha.
Nassari inadaiwa alipigwa wilayani Monduli kwenye Kata ya Makuyuni siku moja kabla ya uchaguzi wa udiwani kwenye kata hiyo.
No comments :
Post a Comment