HOTUBA
YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH S. WARIOBA,
KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UZINDUZI WA RASIMU YA
KATIBA TAREHE 03 JUNI, 2013 KWENYE VIWANJA VYA UKUMBI WA KARIMJEE, DAR
ES SALAAM.
Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilali – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
Mhe. Mizengo K. P. Pinda (Mb.) - Waziri Mkuu,
Mhe. Seif Sharif Hamad – Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (Mb.) - Makamo wa Pili wa Rais - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Mathias Chikawe – Waziri wa Katiba na Sheria,
Mhe. Abubakar Khamis Bakary - Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Jaji Frederick M Werema - Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Othman Masoud Othuman - Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume na Wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Ndugu Wananchi,
Wageni Waalikwa
Waandishi wa Habari Mabibi na Mabwana.
UTANGULIZI
Ndugu Wananchi,
Awali ya yote namshukuru mwenyezi
mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya leo ya kuzindua Rasimu ya
Katiba. pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria halfa hii ikiwa ni
mwendelezo wa mchakato muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya nchi
yetu.
Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa
mabadiliko Februari, 2012. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa
mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34 wa Tume
waliteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Tume imepewa miezi kumi na minane kukamilisha kazi
yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi ambayo ilikuwa Mei 2,
2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu yake. Kufuatana
na ratiba hiyo Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika
kipindi cha miezi mitano kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi
hiyo ilifanywa kama tulivyopanga. Tume ilijigawa katika makundi na
ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume ilifanya mikutano
1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337ambao kati ya
hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au
kwa maandishi. Tume pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje
ya nchi kwa njia mbali mbali kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu
maalum za Tume, barua kupitia Masanduku ya Barua ya Tume, Mitandao ya
Kijamii ya barua pepe; facebook ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala
mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi wa simu.
Tume
ilitumia mwezi Januari, 2013 kukusanya maoni ya makundi mbali mbali
katika jamii, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi za Serikali,
taasisi za dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi, asasi za kiraia na
kadhalika. Makundi zaidi ya 160 yalikutana na Tume na kutoa maoni. Tume
pia ilipata maoni ya viongozi wa juu wa Serikali walioko madarakani na
waliostaafu. Kwa jumla viongozi 43walitoa maoni.
Tume ilipanga kutumia
miezi mitatu ya Februari, Machi na Aprili kuchambua maoni ya wananchi na
kuandaa Rasimu ya Katiba. Lakini tuligundua kwamba maoni tuliyopata
yalikuwa mengi sana, na pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa,
tulitambua umuhimu wa kuongeza muda hadi mwisho wa mwezi Mei, Maoni ya
wananchi yaligusa mambo yote yanayohusu Katiba na mengi ya maoni hayo
yalikinzana. Aidha, baadhi ya maoni yaligusia masuala ya Kisera,
Kisheria na Kiutendaji. Tulifanya uchambuzi makini na wa ndani wa maoni
hayo na kazi hiyo tumeikamilisha na rasimu imeandaliwa na Tume na leo
tupo hapa kwa ajili ya kuizindua, ambapo Wananchi watapata nafasi ya
kuisoma. Kwa leo, kwa niaba ya Tume, napenda kutaja maeneo machache tu
ambayo tunayapendekeza.IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA
Ndugu Wananchi,
Katiba yetu ya sasa ina ibara
152. Tume ilifanya jitihada kubwa sana kuandaa rasimu ambayo siyo ndefu.
Lakini katika hali halisi haikuwezekana. Rasimu ya Katiba
tunayopendekeza ina ibara 240.
MISINGI MIKUU YA TAIFA
Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio unaobeba misingi
mikuu ya Taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Tume inaamini
kwamba misingi hii ni mizito na inastahili kubaki kwenye Katiba mpya.
Hata hivyo, Tume imeona ni busara kuongeza misingi mingine mitatu ya
Usawa, Umoja na Mshikamano. Hivyo, Tume imependekeza Katiba iwe na
Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu, Usawa, Umoja,
Amani na Mshikamano.
TUNU ZA TAIFA
Katiba yetu ya sasa haina sehemu inayoelezea tunu
za Taifa (National Values). Wananchi wengi walitoa maoni kwamba Katiba
itaje Tunu za Taifa. Tume imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani ya
Katiba. Tunu hizo ni;- Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi,
Uwajibikaji na Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.
MALENGO YA TAIFA
Tume ilipozunguka nchi nzima wananchi walizungumzia
sana kuhusu malengo ya taifa. Walitaka Katiba ionyeshe dira ya taifa.
Wananchi wanayo ndoto yao ya Tanzania ya kesho na kesho kutwa. Kwa
kuzingatia maoni ya wananchi, kuna sura nzima inayohusu Malengo mahsusi
na ya msingi ya mwelekeo wa shughuli za Kiserikali na Sera za Kitaifa.
Rasimu ya Katiba inaeleza kuwa Malengo ya Kitaifa yaliyoainishwa ndani
ya Rasimu yatakuwa ni Mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, Vyama vya
Siasa, Taasisi na Mamlaka nyingine, na kwa kila mwananchi katika
matumizi au kutafsiri Masharti ya Katiba au Sheria nyingine za Nchi.
Kwa
msingi huo, Tume imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa
mpangilio wakuonesha malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni,
kimazingira na sera ya mambo ya nje. Malengo hayo yameingizwa kwenye
Rasimu ya Katiba.
VYOMBO VYA KIKATIBA
Wananchi walizungumzia suala la kubainishwa kwa
vyombo vya Kikatiba na kuingizwa kwenyeKatiba ili viwe na nguvu ya
Kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yao. Tume imependekeza baadhi ya
vyombo vifuatavyo viwe vya Kikatiba; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa
Serikali, Baraza la Mawaziri, Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na
Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri; Baraza la Ulinzi na Usalama la
Taifa, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya
Utumishi wa Umma, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora
MAADILI YA VIONGOZI NA MIIKO YA UONGOZI
Wananchi wengi pia walizungumzia kwa upana sana
kuhusu maadili na miiko ya Viongozi, kwa kuzingatia maoni ya
wananchi Tume inapendekeza maadili ya viongozi wa umma, pamoja na miiko
ya uongozi yawekwe kwenye Katiba. Tume pia imependekeza kuwaSekretariati
ya Maadili ibadilishwe kuwa Tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia
maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.
HAKI ZA BINADAMU
Kuhusu haki za binadamu wananchi walitaka haki hizi
ziimarishwe na kusiwe na vikwazo visivyo vya lazima. Tume imependekeza
mabadiliko katika baadhi ya haki za binadamu kwa madhumuni ya
kuziimarisha. Moja ya mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru wa mwananchi
kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza kwamba vikwazo
vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume
inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.
Tume pia, inapendekeza haki
mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, ,
haki ya mtoto, haki za Watu wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za
Wazee, Haki za Makundi Madogo katika Jamii, Haki ya Elimu na Kujifunza,
Haki ya kupata habari, Haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na
kadhalika.
URAIA
Wananchi wengi walipendekeza kuwa suala la Uraia
libainishwe wazi kwenye Katiba. Tume imependekeza kwa kutaja Raia wa
Jamhuri ya Muungano na haki zake.
MIKOPO NA DENI LA TAIFA
Ndugu Wananchi,
Wananchi walizungumzia suala la
uwepo wa Ukomo wa nchi kukopa na uwepo wa utaratibu wa kulipa Deni la
Taifa ili kuilinda Nchi isiwe na deni kubwa. Kwa kuzingatia maoni ya
Wananchi, Tume imependekeza kuwa, Serikali itawajibika kutoa taarifa
Bungeni kuhusu Mikopo kwa kuainisha kiasi cha deni lililopo, riba yake
na matumizi ya fedha za Mikopo na utaratibu wa kulipa Madeni ya Taifa.
MFUMO WA UTAWALA
Kuhusu utawala, Tume inapendekeza Tanzania iendelee
na mfumo wa Jamhuri kwa maana ya nchi inayoongozwa na Rais Mtendaji
ambaye ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
UCHAGUZI WA RAIS
Umri wa kugombea Urais
Tume ilipokea maoni yanayokinzana kuhusu umri wa
mwananchi kugombea Urais. Baadhi walipendekeza mtu akishakuwa na sifa ya
kupiga kura awe pia na sifa ya kugombea Urais. Umri wa mtu kuruhusiwa
kupiga kura ni miaka 18. Wengine walipendekeza umri uliopo kwenye Katiba
wa mtu kugombea Urais, yaani kuanzia miaka 40 na kuendelea, uendelee
kubaki kama ulivyo.
Wengine walisema Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea
Urais uwe miaka 35 au miaka 50 na kuendelea.
Tume imeyachambua maoni
yote hayo, ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za Nchi zingine na
uhalisia wa watu wanaogombea na kuchaguliwa kuwa Marais katika Nchi
mbalimbali Duniani ambazo zingine zimeruhusu wagombea wa nafasi ya Urais
kuwa na umri chini ya miaka 40.
Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo
walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi.
Kwa kuzingatia maoni ya
wananchi, utafiti na hali halisi, Tume inapendekeza Rais aendelea
kuchaguliwa na wananchi na pamoja na sifa nyingine, mtu anayeomba urais
asiwe chini ya miaka 40.
Uchaguzi wa Rais itakuwa kama ilivyo sasa,
yaani mgombea Urais atakuwa na mgombea mwenza kwa utaratibu kama ilivyo
sasa. Isipokuwa, Tume imependekeza Mgombea Urais anaweza kupendekezwa na
Chama cha Siasa au kuwa Mgombea Huru.
Mgombea wa nafasi ya Rais
atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia
hamsini ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa
Rais yanaweza kulalamikiwa Mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza
kufungua kesi. Wanaoweza kufungua kesi ni wagombea Urais. Aidha, ni
Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na Mamlaka na uwezo wa kusikiliza
malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe
ndani ya mwezi mmoja, yaani siku therathini.
Rais aliyeshinda
ataapishwa siku thelathini tangu alipotangazwa kuwa mshindi au
kuthibitishwa na Mahakama.
MADARAKA YA RAIS
Ndugu Wananchi,
Tume inapendekeza kwamba, Rais
abaki na madaraka ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Hata hivyo
inapendekezwa Rais ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika
uteuzi. Kwa mfano:
Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais atateua
na Bunge litathibitisha.
Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu Rais
atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya
Uutumishi wa Mahakama na baada ya hapo Bunge litathibitisha.
Kuhusu
Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama inapendekezwa kianzishwe chombo
kipya kitakachoitwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, ambalo kati ya
majukumu yake itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama.
Kuhusu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa
Umma.
KINGA YA RAIS
Tume baada ya kupitia maoni ya Wananchi,
inapendekeza Rais abaki na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushitakiwa
na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.
IDADI YA MAWAZIRI
Inapendekezwa Rais aunde Serikali ndogo iliyo
na Mawaziri wasiozidi kumi na tano na mawaziri hao wasiwe wabunge.
Mawaziri hawatahudhuria vikao vya Bunge isipokuwa kama watahitajika
kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.
BUNGE
Ndugu Wananchi,
Kuhusu Bunge kutakuwa na wabunge wa
aina mbili. Kutakuwa na Wabunge wa kuchaguliwa na wabunge watano wa
kuteuliwa na Rais kuwakilisha Watu wenye Ulemavu.
Kila Jimbo la
Uchaguzi litakuwa na Wabunge Wawili mmoja mwanamke na mwingine
mwanamume.
Tume inapendekeza kwamba, Mbunge akifukuzwa na Chama cha
Siasa abaki kuwa Mbunge lakini akihama Chama atapoteza Ubunge
wake.
Inapendekezwa ukomo wa Ubunge uwe vipindi vitatu vya miaka
mitano mitano. Hata hivyo,wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kabla
ya mwisho wa kipindi chake.
Inapendekezwa pia kusiwepo na uchaguzi
mdogo isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na Mbunge huru
ndipo utafanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo, lakini kama nafasi
ikiwa wazi kutokana na Mbunge wa Chama cha Siasa basi nafasi hiyo,
ijazwe na mtu kutoka Chama hicho.
Inapendekezwa Spika na Naibu Spika
wasitokane na Wabunge na wasiwe Viongozi wa vyama vya Siasa.
TUME YA UCHAGUZI
Tume imefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi kuhusu
Tume ya Uchaguzi. Tume inapendekeza jina la tume liwe Tume Huru ya
Uchaguzi. Tume pia inapendekeza sifa za wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi
ziwekwe kwenye Katiba. Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watapatikana
kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya Katiba kwa
kuomba. Majina ya waombaji yatachambuliwa na Kamati ya Uteuzi ambayo
Mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni
Majaji Wakuu wa nchi Washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano,
Maspika wa Mabunge wa nchi Washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu.
Kamati ya uteuzi itapendekeza majina ya watu wanaofaa kwa
Rais ambaye atateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine.
Bunge litathibitisha uteuzi wao. Wabunge na viongozi wa aina hiyo
hawatakuwa na sifa za kuwa wajumbe wa tume ya uchaguzi.
Inapendekezwa
Tume huru ya Uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na
Usajili wa Vyama vya Siasa.
MAHAKAMA
Kuhusu Mahakama inapendekezwa kuanzishwa kwa
Mahakama ya Juu (Supreme Court) Majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya
Rufani watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
MUUNDO WA MUUNGANO
Ndugu Wananchi,
Suala la muundo wa Muungano ndilo
lililokuwa gumu kuliko masuala yote. Tume ilitumia muda mwingi kuchambua
maoni ya wananchi. Pamoja na kwamba hadidu za rejea zilielekeza Tume
kuzingatia uwepo wa Muungano, baadhi ya wananchi walitoa maoni kwamba
Muungano uvunjwe na Tume iliyapokea maoni hayo. Licha ya kwamba
waliotaka kuvunjwa muungano walikuwa wachache sana, Tume ilichambua
sababu walizotoa na kuridhika kwamba hazikuwa na uzito.
Wananchi walio
wengi walitaka Muungano uendelee. Kati yao wapo waliopendekeza Muungano
wa Serikali moja, Serikali mbili, Serikali tatu, Serikali nne na
muungano wa mkataba. Sababu za wale waliopendekeza Serikali nne hazikuwa
na uzito, kwa hiyo Tume ikaamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi
waliopendekeza Serikali moja walikuwa wachache lakini sababu zao zilkuwa
na uzito. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia hali halisi iliona ni
changamoto kubwa kuwa na Muungano wa Serikali Moja.
Wananchi
waliopendekeza Muungano wa Mkataba walikuwa wengi (hasa wananchi wa
Zanzibar) na sababu zao zilikuwa na uzito. Lakini uchambuzi wa Tume
ilionekana wazi kwamba ili kupata mkataba lazima kwanza kuwe na nchi
mbili huru kabisa lakini hakukuwa na mazingira ya uhakika ya kupata
mkataba wa muungano. Tume iliona kuna changamoto ya muungano kuvunjika
ingawa waliotoa maoni walisisitiza muungano ubaki. Hivyo, Tume iliamua
kutopendekeza muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Tanzania iendelee na
Muundo wa sasa wa Serikali mbili walikuwa wengi na sababu zao zilikuwa
nzito. Hata hivyo, wananchi katika kundi hili walipendekeza mabadiliko
mengi na makubwa. Tathmini ya Tume ilionyesha kwamba isingewezekana
kufanya mabadiliko yote yaliyopendekezwa.
Wananchi waliopendekeza
muundo wa Serikali tatu walikuwa wengi kuliko makundi yote. Sababu zao
zilikuwa nzito lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi na nzito. Pamoja
na maoni ya wananchi Tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo huu
zilizotolewa na Tume zilizopita na Tafiti zilizofanywa na Tume kuhusu
aina mbalimbali za Muungano. Baada ya yote hayo Tume ilifikia uamuzi wa
kupendekeza mfumo wa Serikali tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho,
Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO
Ndugu Wananchi,
Tume imependekeza katika Rasimu ya
Katiba kuwa orodha ya Mambo ya Muungano yawe 7 badala ya 22 yaliyopo
sasa.
Mambo ya muungano yanayopendekwa ni:
Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Uraia na Uhamiaji
Sarafu na Benki Kuu
Mambo ya Nje
Usajili wa Vyama vya Siasa
Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
BENKI KUU
Kwa kuwa Tume imependekeza Muungano wa Shirikisho
kutokana na uzito wa maoni ya wananchi. Hivyokutakuwa na Benki Kuu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa nawajibu wa kusimamia
masuala ya Sarafu na Fedha za Kigeni na Benki za Washirika wa Muungano.
BENKI ZA SERIKALI ZA WASHIRIKA
Kutokana na pendekezo la kuwepo kwa Serikali ya
Shirikisho la Nchi tatu, inapendekezwa kuwepo kwa Benki zitakazokuwa na
jukumu la kutunza akaunti ya fedha za Serikali za kila Mshirika wa
Muungano na kuzisimamia benki za biashara katika mamlaka zao.
BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU YA KATIBA
Serikali ya Majimbo
Ndugu Wananchi,
Tume ilipokea maoni kuhusu mambo
mengine muhimu ambayo hayamo katika rasimu hii. Moja ya mambo hayo
ni Serikali za Majimbo. Tume ilichambua maoni na sababu za wananchi
kupendekeza Serikali za Majimbo lakini Tume ilibaini changamoto nyingi
na ikaamua kutopendekeza muundo huu.
Kwanza, baada ya kuamua
kupendekeza Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, ilionekana ni dhahiri
kuongeza ngazi nyingine ya Serikali ingeleta gharama kubwa. Serikali
nyingine kumi zingekuwa na Wakuu wa Majimbo, Mabaraza ya Mawaziri na
Mabunge nagharama yake ingekuwa kubwa.
Pili, katika kutembelea nchi
Tume ilishuhudia dalili za wazi za mivutano ya Udini, ukanda,malalamiko
ya upendeleo wa baadhi ya maeneo na ukabila. Dalili zilikuwa wazi
kwamba utawala wa majimbo ungeirudisha nchi kwenye utawala utakaoigawa
nchi kwa misingi ya ukabila, udini na ukanda na kuzigawa rasilimali za
taifa kikanda na hivyo kuleta tofauti kubwa ya kimaendeleo katika nchi.
Mahakama ya Kadhi
Ndugu wananchi,
Jambo la pili ni mahakama ya
kadhi. Tume ilipokea maoni mengi kuhusu suala hili. Baadhi ya wananchi
walitaka mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba na wengine walipinga.
Baada ya kuamua kuwa Muundo wa Muungano uwe wa Serikali Tatu, Tume
iliona kuwa Mahakama ya Kadhi siyo suala la Muungano na imeliacha
ili lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
Hata hivyo ilionekana kuwa
suala siyo kuwapo au kutokuwapo kwa mahakama ya kadhi.Mahakama hizo
zinaweza kuwapo bila ya kuwa katika Katiba. Zanzibar kuna mahakama ya
kadhi bila kuingizwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Kwa kutumia uzoefu huo
hata Tanzania Bara inaweza kupata ufumbuzi wa suala hili.
Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
Jambo la Tatu ni Kuwepo au kutokuwepo kwa Wakuu wa
Mikoa na Wilaya. Baadhi ya Wananchi walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya
wasiwepo, wengine walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kuwepo
lakini wachaguliwe na wananchi na waengine wakasema wawepo na waendelee
kuteuliwa na Rais kama ilivyo sasa. Tume ilitafakari kuhusu suala hili
na kuamua kwamba siyo suala la Muungano na kwa kuwa Muundo wa Muungano
imependekezwa uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona suala la uwepo au
kutokuwepo na namna ya upatikanaji wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya
lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
Serikali za Mitaa
Kuhusu Serikali za Mitaa, Tume ilipokea maoni
kutoka kwa wananchi kuhusu kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa
kuzipatia uhuru kamili wa kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa na
Serikali Kuu. Tume ilitafakari suala hili na kuamua kwamba siyo jambo la
Muungano na hivyo, litashughulikiwa kwenye Katiba za Washirika wa
Muungano.
Uraia wa Nchi mbili
Ndugu Wananchi,
Jambo la tatu ni Uraia wa Nchi
mbili. Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kuwekwa
kwenye Katiba suala la Uraia wa nchi mbili. Baada ya kufanya uchambuzi
kwa kutengenisha mambo yapi ni ya Kikatiba na yapi yanaweza kutekelezwa
bila kuingizwa kwenye Katiba bali kwenye Sheria inayohusu jambo
husika, Tume imependekeza kuwa suala la Uraia wa nchi mbili linaweza
kuwekwa kwenye Sheria badala ya kuwekwa kwenye Katiba. hii ni kwa sababu
kutokana na utafiti uliofanywa na Tume, suala hilo linaweza kubadilika
wakati wowote na hivyo likiwa kwenye Katiba linaweza kuifanya Katiba
kubadilishwa mara kwa mara.
MWISHO
Naomba nichukue fursa hii kwa niaba
ya Tume kuwashukuru Watanzania wote kwa kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, kuanzia hatua ya kutoa maoni na
kuwachagua wawakilishi wenu watakaopata fursa ya kuipitia, kuijadili na
kuitolea maoni Rasimu ya Katiba. Ushirikiano huu ulikuwa muhimu sana kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba hasa ukizingatia kuwa lengo ni kupata
Katiba Mpya ambayo itaakisi ndoto na matakwa ya Wananchi wa
Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inatoa shukrani za dhati kwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar:
Kwa kuipatia vifaa afisi na mahitaji ya lazima
Kwa kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu,
Kwa kutokuingilia Uhuru wa Tume wakati wa Utekelezaji wa Majukumu yake na
Kutoa Wataalam wenye Weledi, Mahiri, Makini na Waadilifu ambao wameunda Sekretarieti ya Tume.
Ndugu Wananchi,
Shukrani za pekee ziwaendee:
Wakuu wa Mikoa,
Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi / Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya,
Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na Masheha.
Kwa kuisaidia Tume kutekeleza Majukumu yake kwa
ufanisi. Aidha, tunazishukuru Asasi za Kiraia, Taasisi, Jumuiya za
Kidini, Vyama vya Siasa na Makundi mbalimbali kwa namna walivyoshiriki
katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutoa maoni.
Mwisho ingawa
siyo kwa umuhimu, Tunawashukuru Wanahabari wote kwa kazi nzuri
waliyoifanya ya kuisaidia Tume kufikisha taarifa mbalimbali za Tume kwa
Wananchi na katika kuhamasisha Wananchi kushiriki katika mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba.
Nachukua nafasi hii kuwaomba Wananchi kupitia
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi ya Watu wenye Malengo yanyofanana kushiriki vyema, kwa umakini,
utulivu na kwa amani katika hatua hii ya kuipitia, kuijadili na kuitolea
maoni Rasimu ya Katiba.
Tume imekuwa ikithamini na itandelea
kuthamini mawazo na maoni kutoka kwa Watanzania wote.
Rasimu ya Katiba
itapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya www.katiba.go.tz SASA NAKUOMBA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS UIZINDUE RASMI RASIMU YA KATIBA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments :
Post a Comment