Utabiri wa wengi kuwa ushosti wa waigizaji masistaduu wa Bongo Movies,
Wema Isaac Sepetu na Kajala Masanja kutumbukia nyongo unadaiwa kutimia
na sasa wametibuana, Habari
za ndani kutoka kwa mtu wa karibu (jina linahifadhiwa), mwanzoni baada
ya Wema kumlipia Kajala faini ya Sh. milioni 13 na kumnusuru
kutokwenda Segerea a.k.a Segedansi, wawili hao walikuwa marafiki kama
pete na kidole.
“Walishinda wote, walilala wote, walikwenda klabu wote yaani Kajala
alikuwa anamnyenyekea ‘madam’ Wema kwa kumuepusha na kifungo cha miaka 7
jela,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Kuna wakati hapa katikati Kajala alikuwa kama katibu muhtasi wa madam, si unajua lazima atumikie fedha za watu?
“Kabla hajaenda Mwanza kwa ajili ya mapumziko kwa bibi zake, nilimsikia
Kajala akilalama kuwa madam aliamka siku moja akawa amemchunia,
unaambiwa hata salamu ikawa hakuna. “Hapo ndipo maneno ya pembeni yakaanza kwa sababu mbali na Kajala,
Wema pia ana wapambe wengine na mbali na Wema, Kajala naye ana kampani.
Kwa hiyo sosi ya manenomaneno ni hizo kampani zao.
“Ipo siku kabisa Wema alimlalamikia Kajala hadharani kuwa amekuwa akimsema vibaya kwa watu.
“Yale maneno yalimuuma sana Kajala, ikabidi arudi nyumbani kwao lakini
akawa anaogopa kumwambia mama yake kuwa ametibuana na Wema hadi
alipotimkia Mwanza. “Lakini kabla ya hii ishu ya kulaumiana, kipindi cha nyuma kidogo
Kajala alipata dili la kwenda kurekodi filamu nchini China na mastaa
wengine lakini ikadaiwa kuwa Wema alichomoa hivyo mwigizaji huyo
hakwenda pamoja na kwamba alishapewa baraka zote na baba yake.
“Unaambiwa alikuwa amekamilisha taratibu zote za kwenda China, hadi
tiketi alikuwa ameshakata lakini suala hilo lilipotua kwa Wema,
ilidaiwa kuwa alikataa kumruhusu.
TATIZO MILIONI 13? “Mimi nakwambia zile milioni 13 zinamkosesha raha Kajala hadi unamuona kabisa kwamba ana stress (msongo wa mawazo). “Wewe fikiria, kazi inayomwingizia mkwanja ni filamu, sasa unaambiwa
inadaiwa kuwa madam hataki acheze filamu za watu wengine, sasa ataishije
jamani?
“Mimi nakwambia ndiyo maana ameamua kwenda kupumzika Mwanza baada ya kuwa wananuniana kwa kwenda mbele.”
Baada ya kupata habari hizo, mwandishi wetu alimtafuta Wema kwa njia ya
kilongalonga chake cha kiganjani ili kupata undani wa sakata hilo lakini
hakupatikana hewani.
Baadaye mwanahabari wetu alisaga lami hadi kwa staa huyo Kijitonyama,
Dar, alipogonga geti alitoka mlinzi aliyedai kuwa ‘malkia’ alikuwa
ndani amelala na hakuhitaji usumbufu pamoja na kwamba ilikuwa saa 6:30
mchana.
Hata hivyo, mwanahabari wetu alibisha hodi ofisini kwa Wema,
Mwananyamala-Komakoma ili kuzungumza na meneja wake, Martin Kadinda
ambaye alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli Kajala yupo Mwanza,
aliomba ruhusa ya kwenda kupumzika tukampa. Hayo mengine ya kutibuana
na madam siwezi kuyasemea kwa sababu yapo nje ya uwezo wangu.
“Lingekuwa ni suala la kazi hapo sawa lakini ni vizuri ukazungumza na
mkurugenzi mwenyewe (Wema) lakini sidhani kama ataweza kuzungumza kwa
sababu alikuwa anaumwa, amezidiwa na kupelekwa hospitali.”
Alipoulizwa Wema anaumwa nini, Kadinda alifunguka: “Sijajua lakini
ugonjwa ni siri kati ya mhusika na daktari, cha msingi wewe ujue tu
anaumwa.”
Baada ya kupita kote huko kusaka undani wa sakata hilo, mwandishi
alimgeukia Kajala kwa njia ya simu ya mkononi akiwa jijini Mwanza na
kumuuliza kulikoni kutibuana na Wema. Huku sauti ikiwa chini,
Kajala alisema: “Ni kweli kuna hali ambayo hata mimi mwenyewe nashindwa
kuelewa lakini siwezi kuzungumzia kwa leo nikiamini yatapita.”
No comments :
Post a Comment