Wadau, safari ya kupambana na ufisadi katika nchi hii ni ngumu sana. Leo
kuanzia saa 5 hadi saa 8:30 mchana, Mhariri Mtendaji wa Jamhuri, Deo
Balile, amehojiwa Makao Makuu ya Polisi kuhusu habari iliyochapishwa
kwenye Jamhuri inayohusu "Ufisadi ujio wa marais 11".
Kwa bahati nzuri, habari nzima wanaikubali kwamba ni ya kweli! Kasoro
pekee eti ni matumizi ya barua ya Ikulu iliyokuwa na neno "Secret"
ambayo ilikuwa na majina tu. Anashitakiwa kwa kosa la "Kuchapisha
Nyaraka za Siri", jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Usalama, kifungu
5(1). Nimemwekea dhamana hadi Ijumaa saa 4 asubuhi.
Hii ndio habari Iliyosababishwa kuhojiwa hii hapa
Ufisadi wa kutisha ujio marais/Obama: Zaidi ya Bilioni 8 zatumika!
- Hazina yatumia Shilingi bilioni 8
-
Wajanja’ watafuna mamilioni
-
Vifaa vya Obama vyaokoa jahazi
-
Vinyago vyagharimu Sh milioni 30
-
Sare, mikoba, vyagharimu mil. 400/-
-
Karamu, chupa za kahawa, miavuli mil. 390/-
-
Burudani ya muziki yatafuna milioni 195
Na Waandishi Wetu
Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote
(Smart Partnership Dialogue), uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, umeigharimu Serikali Sh bilioni nane.
Hata hivyo, mamilioni ya fedha hizo yameishia mikononi mwa watumishi
kadhaa wa Serikali kupitia zabuni tata walizotoa kwa kampuni mbalimbali.
Baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa kwenye zabuni hizo, ama
havikuwasilishwa, au viliwasilishwa shughuli ikiwa imeshamalizika, na
sasa vimetunzwa kwenye maghala. Miongoni mwa vifaa hivyo ni shehena
kubwa ya bendera za Tanzania ambazo zimetunzwa katika chumba ndani ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.Wahusika wakuu kwenye
ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni huo. Katibu wa Bodi ya Zabuni
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Onesmo Suka,
ni miongoni mwa maofisa wanaokabiliwa na wakati mgumu kueleza mchanganuo
wa zabuni ulivyokwenda.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umeonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha
cha Sh bilioni nane ni mbali kabisa na kile kilichokusanywa kutoka
kampuni na mashirika mbalimbali ya umma.
Imebainika kuwa hadi Juni 5, mwaka huu, fedha taslimu zilizokusanywa ni
Sh milioni 170 kutoka kampuni saba. Wachangaji wa kiasi hicho na kiwango
kikiwa kwenye mabano ni Kampuni ya Simu ya Tigo (Sh milioni 80), PPF
(Sh milioni 20), PSPF (Sh milioni 20) na LAPF (Sh milioni 20). Benki Kuu
(BoT) ilitoa Sh milioni 10, Barrick Gold (Sh milioni 15) na Benki ya
Azania (Sh milioni 5).
Kampuni tatu zilikubali kutoa vifaa. Vodacom iliamua kuchangia masuala
ya ICT, Masasi Foods walitoa maji ya kunywa, ilhali Shirika la Hifadhi
la Taifa (TANAPA) lilitoa fulana na zawadi ndogo ndogo.
Hadi Juni 5, mwaka huu, kampuni tano zilikuwa zikisubiri uamuzi wa Bodi.
Kampuni hizo ni Mac Group, CBA Bank, PBZ Bank, Nokia-Siemens na Shirika
la Hifadhi la Taifa (NSSF).
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni nne zilishindwa
kuchangia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni uwezo wake mdogo kifedha.
Kampuni hizo ni TanzaniteOne inayochimba tanzanite Mererani; IBM,
Infrotech ba Diamond Trust Bank.
Wafanyabiashara nguli nchini hawakuachwa nyuma kwenye michango hiyo,
ingawa taarifa zinasema wapo waliokataa kutoa. Mwenyekiti wa Kamati ya
Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya
Wote, Balozi Ombeni Sefue, aliagiza wafanyabiashara kama Said Bakhresa
na Mohamed Dewji wafuatiliwe kwa karibu ili waweze kutoa michango.
Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership
Dialogue, Victoria Mwakasege, anasema kwamba baadhi ya wafanyabiashara,
wakiwamo kina Dewji, hawakuchangia. Hakutoa sababu za kushindwa kwao.
Sokomoko la matumizi mabaya ya fedha
Uchunguzi umethibitisha kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya
Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na
namna zabuni zilivyotolewa.
Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye
ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na
mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.
Sefue amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo
kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya fedha
yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17,
vinasema Balozi Sefue, aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu
za ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kwamba baadhi ya vitu
vilivyoorodheshwa, vilikuwa ni “vichekesho”.
“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe
wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonyesha nini kinanunuliwa
kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha vitu na kuweka
gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.
Kampuni zilizopata zabuni
Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
wamesema wazi kwamba fununu za kufanyika kwa mkutano wa Smart
Partnership zilipoenea, watu wengi walipigana vikumbo wakitaka wapewe
zabuni.
Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu
mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1 Baadhi ya vitu hivyo ni
vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa
protoko, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na
wageni wa kawaida, na beji.Kampuni ya Softel Trading Company Limited
ilipewa zabuni ya Sh milioni 392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini,
miavuli (1,500), chupa za kahawa (800), vikombe vya kahawa (800), kalamu
za zawadi (2,000) na vishikio vya funguo (800).
Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili
ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa mabango
madogo madogo.
Kana kwamba haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd
ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza
mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam,
iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es Salaam,
Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.
Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409,269
kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu
masuala ya kiasiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano,
usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.
Kampuni ya tano iliyoshinda zabuni ni ya Big Mama’s Woodworks ambayo
ilipangiwa Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za vinyago
60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila kimoja. Pia
ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyanye urefu wa sentimita 150 na
upana wa sentimita 35.
Kwenye masuala ya burudani, kampuni ya Prime Time Promotion ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7.
Kwenye orodha ya ugawaji zabuni, kampuni ya True Colour Entertainment
Group ilizawadiwa zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kuandaa na
kuonyesha jarida. Ingawa haikufafanuliwa, hii yawezekana ndilo lile
jarida lililoonyeshwa kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu
Nyerere, siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Smart Partnership. Lilihusu
wanyamapori na vivutio kadhaa vya utalii vinavyopatikana hapa nchini.
Zabuni ya nane ilitolewa kwa kampuni ya Simply Computers (T) Ltd.
Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa mbili,
idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.
Kampuni hiyo hiyo ya Simply ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya Sh
milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani, laptop
(5), laptop za sekretarieti na mkutano (14), mobile computing equipment
(14), black and white printer (2), colored printer (2), kompyuta za
mezani (nyingine 5), colored printer (nyingine 2) na flash disk (32).
Upungufu uliojitokeza
Pamoja na mamilioni hayo kupitishwa kwa ajili ya mkutano huo lakini bado
kulikuwa na upungufu mkubwa katika utendaji hususani katika utoaji wa
vitambulisho.vitabulisho wa
JAMHURI lilishuhudia baadhi ya wageni wakiwemo mabalozi kutoka katika
mbalimbali Askari wa Jeshi la Polisi usalam wa taifa madereva wa Idara
mbalimbalia za Serikali wakiendelea kusota kwa ajili ya kupata
vitambulisho hivyo .
Kadhia hiyo pia ilimpata Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue ambaye alifika
katika Ukumbi wa Kalimjee saa nne asubuhi ambapo wafanyakazi wa
waliokuwa wakihusika na utoaji wa vitambulisho hawakumjali jambo
ambalo liliwasahangaza wengi waliokuwepo hapo.
Wengi wao walihoji uelewa wa wahudumu hao katika utendaji wao na kama
kweli walikuwa hawamjui kiongozi huyo au ilikuwa ni dharau.
Sefue alikaa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa na kuondoka katika
ukumbi huo huku akiwa hana kitambulisho hadi anaingia ukumbini wa
Kimataifa wa Walimu Nyerere. Saa kumi jioni.
Wengine waliofika katika ukumbi huo na kupata kadhia hiyo ni Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana na mwenzake
ambaye JAMHURI hailikufanikiwa kupata jina lake
Dk. Bana na mwenzake walifika na kujitambulisha kwa mmoja wahudumu
katika ukumbi huo lakini mhudumu huyo baada ya kutekeleza shida yao,
alianza kueleza matatizo yaliyoikumba idara hiyo ya vitambulisho.
“Jamani idara hii ina matatizo kwani hatukuwa tumejipanga kila mtu
yuko kivyake ndio maana mnaona huduma imesimama kama mnavyoona hakuna
majina hapa, mafaili yako tupu na wahusika hawapo kinachotakiwa ni
kufika hapa na kuhakikisha jina lako na pia unakwenda kupiga picha pale
lakini hadi sasa hatujapata majina je nyinyi mlijiandisha,” anasema
mhudumu huyo.
Hata hivyo kauli hiyo ilimuudhi, Dk. Bana na mwenzake hivyo alimtaka
mhudumu huo kutozungumza upungufu wa idara hiyo mbele ya wageni
waliofika katika ukumbi huo, kwani kufanya hivyo ni aibu na haukuwa
wakati wake kinachotakiwa kutoa vitambulisho.
Mhudumu huyo ambaye JAMHURI halikufanikiwa kupata jina leke alionekana
kukerwa kauli hiyo aliendelea kuzumgumzia upungufu huo pamoja na Dk.
Bana mwenzake kunyamaza. Waliondoka katika eneo hilo kwa miadi ya kurudi
baadae.
Viongozi ‘warushiana mpira’
Utata kuhusu uhalali wa fedha zilizotumika kununua vitu hivyo, usiri
kwenye utoaji zabuni na upungufu mkubwa uliojitokeza kwenye shughuli
nzima ya mkutano huo, ni mambo yanayowasumbua sasa viongozi serikalini.
Wakati Katibu Mkuu Kiongozi akijitoa kwenye sakata hilo na kumsukumia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John
Haule; Haule anasema yeye hahusiki. Badala yake anasema anayepaswa
kuulizwa mambo yote yalivyokwenda ni Mkuu wa Sekretarieti ya Smart
Partnership Dialogue, Mwakasege.
Kwa upande wake, Mwakasege anaruka kwa kusema Sekretarieti ambayo yeye
alikuwa Katibu haikuhusika kwa namna yoyote na masuala ya zabuni.
Akasisitiza kwa kusema, “Huyo anasema uniulize mimi (Haule), mwulize
yeye. Mimi nilihusika na logistic, sisi tulipeleka mahitaji, kwenye
zabuni hatukuhusika kabisa. Kilichofanyika ni sisi kukabidhiwa vitu
kulingana na mahitaji. Yeye ndiye mwenye masurufu, ndiye anayejua hesabu
zote za wizara.”
CHANZO: Gazeti JAMHURI
Ifikemahali polisi wetu nao wajitambue.
ReplyDelete