Obama: Tunataka Uwazi wa Mikataba. Omba radhi Kwa mauaji ya Lumumba
Hatimaye Barack Obama, Rais wa Marekani anatembelea tena bara la
Afrika. Hii itakuwa ni mara ya pili Obama kutembelea Bara hili alikotoka
baba yake baada ya ziara yake ya kwanza mwaka 2009. Mwaka huo
alitembelea Ghana na Misri ilhali mwaka huu anatembelea Senegali, Afrika
Kusini na Tanzania. Ziara hiyo itakayoanza tarehe 26 mwezi Juni,
itamfikisha Tanzania tarehe 1 Julai na kuondoka siku ya pili yake.
Uchaguzi wa Obama kuwa Rais wa Marekani ulipokolewa kwa shangwe
Afrika nzima. Wakati Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alilia kwa
furaha, nchi ya Kenya ilitangaza siku ya mapumziko na Rais wa zamani wa
Afrika Kusini ndugu Nelson ‘Madiba’ Mandela alisema ‘ushindi wa Obama
unawafanya Waafrika wathubutu kuota ndoto (Jarida la The Economist).
Hapa Tanzania kulikuwa kuna shamra shamra za kila namna na magazeti
yaliweka vichwa vya habari kana kwamba ni Rais wa Tanzania
aliyechaguliwa.
Waafrika walikuwa na matumaini makubwa sana na bwana Obama. Yamefikiwa?
Ni vema ifahamike kuwa Barack Obama ni Rais wa Marekani na siku zote
atalinda maslahi ya Marekani tu. Kuwa na matumaini makubwa kwamba labda
yeye angeliweza kuiweka Afrika mbele sana ilikuwa ni kujifurahisha tu
nafsi. Maslahi ya Marekani ni ya kipaumbele kuliko kitu kingine chochote
kwa Rais Obama. Kwa wengi Obama amekuwa kama amewavunja moyo.
Tanzania inapokea kiongozi wa Taifa kubwa duniani wa pili sasa ndani
ya kipindi cha miezi 3 tu. Kwanza alikuja Rais wa China na sasa wiki
hii anakuja Rais wa Marekani. Maneno ya mtaani na kwenye mabaraza ya
majadiliano ni kwamba viongozi hawa wanakuja kugombea maliasili tulizo
nazo kama gesi asilia na madini. Nadhani haya ni maneno ya kusema katika
kupiga soga maana kunyonywa kwa rasilimali hakuhitaji Rais wa Marekani
aje Tanzania. Makampuni yote makubwa yanayochimba dhahabu hapa nchini ni
makampuni ya nje na marais wao hawakuja ili waweze kupata mikataba
minono ya kuvuna utajiri wetu. Katika kitalu namba 2 cha utafutaji wa
mafuta na gesi huko Bahari Kuu kampuni ya kimarekani ya ExxonMobil ina
ubia na kampuni ya Norway ya StatOil. Kampuni hiyo haikusubiri Rais wa
Marekani aje ili wapate mikataba.
Kuna makampuni mengi sana ya kichina yanajenga barabara zetu hapa
nchini yakiwa na mikataba minono sana. Kule Mchuchuma na Liganga kuna
kampuni ya kichina inajiandaa na uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe.
Makampuni yote haya hayakusubiri Rais wao aje.
Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ujio wa Marais mbalimbali nchini ni
ujio wa kujijenga kidiplomasia na wakati mwingine kama sehemu ya kutuma
ujumbe Fulani kwa dunia. Nchi inayotembelewa pia inaweza kuona kuwa
diplomasia yake inaheshimiwa na mataifa yanayoitembelea.
Hata hivyo hii haiondoi ukweli kwamba Obama anakuja kwa ajili ya
maslahi ya nchi yake kama ilivyo kwa wachina walivyokuja. Tumesikia Rais
Obama ataambatana na mamia ya wafanyabishara kutoka Marekani kwa ajili
ya kupata fursa za kuwekeza nchini. Pia tutasikia matangazo kuhusu
msaada wa pili wa Millenium Challenge ambapo Wamarekani wanaendelea
kumwaga pesa nchini kusaidia miundombinu lakini pia kushawishi kuungwa
mkono na nchi zetu kwenye maamuzi Fulani Fulani jumuiya za kimataifa.
Tumesikia Obama atakwenda kutembelea mitambo ya kampuni ya Symbion.
Hii ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele kuwa ni mitumba
na hivyo TANESCO wasiinunue. Hawakununua na badala yake kampuni hiyo ya
kimarekani ikainunua, wakaingia mkataba na TANESCO kuwauzia umeme
unaozalishwa na mitambo hiyo hiyo chakavu. Wakati tunasuburi kulipa
takribani tshs 105 bilioni kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi,
tunasubiri kuona wanasiasa watakaokwenda kumsindikiza Obama kwenye
matembezi hayo ya kutembelea mitambo chakavu.
Kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE
imetangaza kuingia ubia na kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini.
Takribani 400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya
Taifa. Pia sehemu kubwa ya umeme utakaozalishwa Mtwara tayari umepata
soko kwenye kiwanda cha kuzalisha udongo ulaya (simenti) cha bwana
Dangote kule Mtwara. Mtendaji Mkuu wa GE bwana Jeff Immelt ametangaza
kuwa kampuni yake itauza mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
mingi zaidi Afrika Mashariki kuliko Marekani katika kipindi cha miaka
mitatu ijayo. Ni biashara tu!
Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwa ziara ya Rais Obama.
Kwa nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri
kipaumbele hiki watu wengi watakiiunga mkono. Hata hivyo Obama ni lazima
asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata
miakataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo na kulipa kodi
inavyostahili. Makampuni ya mafuta kutoka Marekani hayana historia nzuri
duniani na hivyo ni lazima tulisisitize mapema kabisa. Uwazi wa
mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika
vita dhidi ya Ufisadi na ubadhirifu.
Rais Obama atambue kuwa iwapo Tanzania ingekuwa inakusanya nusu ya
kodi zinazokwepwa na makampuni makubwa yanayotumia mbinu kali, basi
tungehitaji misaada ya Marekani na hapa nchini angekuja kama mbia wa
kweli na sawa katika dunia. Hivyo ni vema aungane na Waziri Mkuu wa
Uingereza kuhakikisha kuwa makampuni makubwa hayatumii ‘tax havens’
kukwepa kodi katika nchi kama Tanzania. Uwazi wa mapato yao na
kilicholipwa kwa Serikali ni vema usisitizwe sana na Obama mwenyewe ili
makampuni yao yasikie na yaache kupora utajiri wa Afrika kiujanja
ujanja.
Mwisho ni vema kama Rais Obama ataomba radhi kwa ushiriki wa
Marekani kwenye mauaji wa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo Patrice
Lumumba. Hivi Tanzania inahangaika zaidi ya uwezo wake kupeleka majeshi
huko mashariki ya Kongo kulinda amani. Waafrika wengi tunaamini kuwa
mauaji ya Lumumba ilikuwa ni kama laana kwa Taifa lile na hivyo limekuwa
ni taifa la vurugu na vita licha ya utajiri mkubwa ulioko nchini humo.
Nyaraka za CIA zinaonyesha dhahiri kuwa Rais wa Marekani wa wakati huo
Lyndon Johnson aliagiza kuuwawa kwa mwanamapinduzi Patrice Lumumba.
Kuwaomba radhi Waafrika na hasa Wakongo kuhusu mauaji ya Lumumba ni
jambo litakaloweza kusaidia sana kurejesha amani Kongo.
Karibu Afrika, Karibu Tanzania ndugu Barack Hussein Obama.
Zitto Z Kabwe
Makala haya yanatarajiwa kutoka kwenye gazeti la MWANANCHI, mfululizo wa makala kuhusu ziara ya Obama.
No comments :
Post a Comment