
Tofauti na Agosti 19, mwaka huu wakati
aliposafirishwa kwa helikopta, jana Sheikh Ponda alisafirishwa kwa
barabara kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro akiwa chini ya ulinzi.
Mbali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Morogoro kufungwa, nyingine ni Hazina Ndogo, Madini, Posta, Vipimo,
Ukaguzi na Maktaba ya Mkoa.
Sababu za kufungwa kwa ofisi hizo pamoja
na Mtaa wa Stesheni na maeneo ya Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo.
Magari yalizuiwa kutembea katika njia na maeneo ya karibu na ofisi
pamoja na Mahakama hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya askari polisi na
magereza kwa muda wote wa takriban saa mbili.
Alifikishwa mahakamani hapo saa 4:10
asubuhi akiwa katika basi la Magereza ambalo lilisindikizwa na jingine
dogo, huku magari mengine yakisimamishwa kupisha msafara huo.
Mahakama hiyo ilifurika umati wa wafuasi
wa kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na wana usalama wengine kuweka
utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo lililokuwa likitumika
kuendesha kesi hiyo.
Shughuli katika eneo hilo zilirejea
katika hali yake ya kawaida saa 6:25 mchana baada kesi yake kuahirishwa
na msafara wa Sheikh Ponda kurejea katika Gereza la Segerea, Dar es
Salaam ambako yuko rumande.
Muda wote tangu kuwasili mpaka
kusikilizwa kwa kesi hiyo, wafuasi hao walikuwa kimya hadi pale
ilipoahirishwa na hasa baada ya Sheikh Ponda kuwapungia mkono alipokuwa
akielekea kwenye basi ambako walisikika wakisema:
“Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu Mkubwa).”
Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali,
Benard Kongola alisema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa
Morogoro, Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa ya uchochezi
Agosti 10, mwaka huu saa 11.45 jioni kwenye maeneo ya Kiwanja cha Ndege,
Morogoro.
Alisema siku hiyo, Sheikh Ponda
alialikwa kutoa maelezo machache kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa
na Umoja wa Wahadhiri Mkoa wa Morogoro (Uwamo) na kwamba akiwa hapo
alitamka maneno:
“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa
kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na
Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), ambao ni vibaraka wa CCM na
Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba
wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na
madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana,” huku akijua kutoa maneno
hayo ni kosa kisheria.
Alisema kwa kufanya hivyo, Sheikh Ponda
anayetetewa na mawakili watatu wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja
masharti ya Mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa imetamka kuhubiri
amani.
Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia:
Serikali ilipeleka jeshi Mtwara
kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka
na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu,
lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu
asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”
Shtaka la tatu ni kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama yalivyo katika shtaka la pili.
Baada ya kusoma mashtaka hayo, Kongola
alisema walikuwa na mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD
mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro(OCD),
Agosti Mosi, 2013 cha kongamano husika na hati ya hukumu iliyotolewa na
Mahakama ya Kisutu, Mei 9, 2013.
Baada ya kusomewa, Sheikh Ponda alikana
mashtaka yote matatu huku akikubali kuwemo kwenye kongamano hilo.
Alikiri kukamatwa na polisi Agosti 11, Dar es Salaam.
Wakili wa utetezi, Nassor aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja akisema mashtaka hayo yote kisheria yana dhamana.
Pia aliwasilisha ombi la kupatiwa hati
yenye maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwani alisema kuwa kutokana na upelelezi upande wa mashtaka kukamilika,
wanahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi.
Hata hivyo, Wakili Kongola aliiomba
Mahakama kutompa dhamana mshtakiwa kutokana na cheti kilichotolewa na
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa
masilahi ya usalama wa nchi.
Akitoa mwongozo wa maombi
yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate aliahirisha kesi
hiyo hadi Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba Septemba
17, mwaka huu Mahakama itatoa uamuzi endapo mshtakiwa atapewa dhamana au
la wakati itakapoanza kusikilizwa.
No comments :
Post a Comment