Jopo la Madaktari Bingwa Saba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH) na Taasisi ya Mifupa ya hospitali hiyo (Moi), wamefanikiwa
kuwatenganisha pacha waliokuwa wameungana kiwiliwili.
Iliwalazimu mabingwa hao kutumia saa nne
kufanikisha upasuaji huo. Mmoja wa watoto hao waliotenganishwa, amelazwa
kwenye Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU) Taasisi ya Mifupa Moi wakati
kiwiliwili kingine kilifariki.
Jopo la madaktari waliofanikisha upasuaji huo ni;
bingwa mstaafu wa watoto ambaye aliitwa maalumu kwa kazi hiyo, Petronila
Ngiloi, Dk Robert Mhina (mifupa) na Profesa Karim Manji aliyekuwa
akifuatilia kwa karibu mapigo ya moyo.
Wengine ni Dk Karima Khalid aliyekuwa akiratibu
dawa ya usingizi, Dk Hamis Shaaban (ubongo na uti wa mgongo), Dk Zaitun
Bokhary (bingwa upasuaji watoto) na Dk Nyangasa (moyo na mishipa ya
fahamu).
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Dk Shaaban
alisema walimfanyia vipimo mtoto ambaye hakuwa amekamilika na
kugundulika kuwa hakuwa amekamilika viungo vyote achilia mbali kutokuwa
na kichwa na macho pia hakuwa na moyo, figo, tumbo, maini ila alikuwa na
uti wa mgongo.
“Uti wa mgongo ulikuwepo na ndio uliokuwa
umeshikana na mwenzake na kuna mshipa mmoja wa fahamu ulikuwa unafanya
kazi ndio maana alikuwa ukimgusa anachezesha mguu.”
Alisema kinachoratibiwa kwa sasa ni kuangalia dawa
ya usingizi aliyopewa mtoto ambaye anaendelea kupumua na kwamba ndani
ya saa 24, dawa ya usingizi waliyomuwekea mtoto huyo itakuwa imeisha na
ataanza kunyonya kama kawaida.
Upasuaji
Kazi ya upasuaji huo ilianza saa mbili asubuhi kwa
mtoto huyo wa jinsi ya kike aliyetimia kuchukuliwa vipimo mbalimbali
ikiwemo CT Scan, MRI, Ultra sound na vingine vingi kabla ya upasuaji
kamili kuanza saa tano asubuhi.
Dk Shaaban alisema ni mara ya kwanza kwa Moi
kufanya upasuaji wa aina ile na kwamba mara nyingi wamekuwa wakifanya
upasuaji wa watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi
ambao tatizo hilo linasababishwa na upungufu wa madini ya folic acid.
Kabla ya upasuaji kuanza, mama wa mtoto huyo Pili
Hija (24) alitumia muda wa nusu saa kufanya maombi maalumu ya kumwombea
mtoto wake kisha kuwaruhusu madaktari kuendelea na upasuaji huo.
No comments :
Post a Comment