Juzi; tuliandikia habari fupi kuhusu ugomvi wa Johari na Chuchu Hans ambao walikuwa wakigombania penzi la Ray..
Katika habari hiyo, tuliahidi kuifuatilia taarifa hiyo kwa kina
zaidi. Bahati nzuri gazeti la AMANI limemaliza kila kitu. Hii
ni ripoti yake.

Waigizaji wenye majina makubwa Bongo, Blandina Chagula ‘Johari’ na
Chuchu Hans wanadaiwa kuchapana kisa kikidaiwa kuwa ni penzi la
mwigizaji ‘kaka mkubwa’, Vincent Kigosi ‘Ray’.
TUHUMA
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini ambacho ni rafiki wa karibu wa wasanii
hao, tukio hilo lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya Ofisi za
RJ Productions, zinazomilikiwa kwa ubia wa Ray na Johari zilizopo
Sinza-Mori jijini Dar ambapo Johari alikuwa akimtuhumu Chuchu mambo
mazito ya kimapenzi kwa Ray.
Shushushu huyo alitonya kuwa, siku ya tukio Johari na wasanii wenzake
walikuwa wakirekodi filamu ndani ya hoteli moja (jina tunalo) iliyopo
jirani na ofisi hizo ndipo alipofikishiwa umbeya kuwa Chuchu yuko kwenye
ofisi hizo ‘akijiachia’ na bosi mwenzake (Ray), jambo lililotia ganzi
moyoni mwa mdada huyo.
MCHEZO MZIMA
‘Kikulacho’ huyo aliendelea kudai kuwa baada ya Johari kupata habari
hizo, bila kujiuliza wala kuvuta subira, ‘alisaga soli’ hadi maeneo
hayo.
“Alipofika aliingia ndani moja kwa moja na kumvamia Chuchu huku akimshushia kipigo chenye ujazo,” kilidai chanzo hicho.
Alidai kuwa katika timbwili hilo, Chuchu naye alifurukuta ndipo
wakazichapa laivu kabla ya Ray aliyekuwa nje kusikia na kuwahi kuokoa
jahazi.
“Unajua kilichomshtua Ray ni kilio cha Chuchu aliyekuwa akiomba msaada baada ya kuzidiwa na Johari,” kilidai.
Chanzo kilidai kuwa aliingia ndani akiwa amefura na kufoka lakini
alikuwa ameshachelewa kwani tayari Johari alikuwa ameshaugeuza bucha
mwili wa Chuchu.
Ilidaiwa kuwa baadaye Ray alimtoa nje Johari akimtaka kuwa mbali na Chuchu.
SINEMA YA BURE
“Ilikuwa ni bonge la soo, watu walijaa sana, baadaye Ray alimtoa Johari nje huku akimfokea.
“Unaambiwa Johari alikuwa akikimbia na Ray kumfukuza, jambo lililovutia
watazamaji wa sinema hiyo ya bure,” alisema mpashaji wetu.
JOHARI, CHUCHU WASAKWA
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, gazeti hili liliwasaka Johari na Chuchu kwa nyakati tofauti.
JOHARI AKIRI
Kwa upande wake Johari alikiri kutokea kwa kasheshe hiyo.
“Ni kweli lakini nani amekuambia? Unajua kilichoniudhi mimi ni maneno
machafu ya huyu dada (Chuchu) anavyotamba kwa watu kuwa amenipokonya
mume, wakati hakuna ukweli juu ya hilo, nilishikwa na hasira sana ndiyo
maana nikaamua kumpa somo kidogo.
“Inaniuma kwa sababu mimi na Ray tumetoka mbali sana hadi kuisimamisha
RJ. Tulikuwa hatuna kitu kabisa tukaungaunga huku na kule hivyo Chuchu
anapaswa kutambua hilo. Asitake kunikumbusha vitu vingi kwa sababu
tuliteseka sana,” alisema Johari kwa uchungu.
VIPI BADO ANAKWENDA RJ?
“Tangu ile ishu itokee sijaenda RJ kwa sababu Ray alinifukuza eti kisa
Chuchu. Usiniulize muafaka wa hili jambo kwa sababu hadi sasa sina
majibu ya moja kwa moja kuna vitu naviweka vizuri,” alisema mwanadada
huyo.
HUYU HAPA CHUCHU
Kwa upande wake Chuchu aliruka kimanga kuwa hakuna ishu kama hiyo.
“Aaah, jamani sina cha kusema juu ya hilo, nikiwa tayari nitawaambia.
“Kinachonishangaza kila Johari na Ray wakigombana huwa natajwa mimi.
Yaani sijui hata haya mambo yanatokea wapi,” alisema Chuchu.
RAY
Gazeti hili lilipomtafuta Ray kutaka kujua ukweli wa ishu hiyo, bila kujibu ndiyo au hapana, alimjia juu mwandishi:
“Sikia Brighton (mwandishi), hili jina nimelitafuta kwa miaka mingi. Nakuomba usiandike habari hiyo, sielewi chochote.
“Ugomvi wao siujui na wakigombana waache kunitaja, waeleze sababu zao za
kugombana siyo kunitajataja mimi,” alisema Ray na hata alipoulizwa
uhusiano wake na wanawake hao aliishia kujiumauma bila kutoa majibu ya
kueleweka.
HALI NI MBAYA
Habari za kina zilidai kuwa hali ni mbaya kati ya mastaa hao ambapo
mashabiki wao waliozungumza na gazeti waliiomba Kamati ya Nidhamu ya
Bongo Movie kuingilia kati ugomvi huo ili kutafuta ufumbuzi.
-Gazeti la AMANI via GPL
No comments :
Post a Comment