WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema yuko imara na hakatishwi
tamaa na maneno ya baadhi ya wanasiasa dhidi ya harakati zake za
kisiasa.
Lowassa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati
akizungumza katika harambee ya ujenzi wa Shule ya Msingi ya Kanisa la
African Inland Church of Tanzania (AICT) mjini Kahama, Mkoa wa
Shinyanga.
Alisema, wanasiasa wanaomshambulia na kueneza mabaya dhidi yake hawambabaishi.
“Si nia yangu kuwajibu hao wanaonisema sema..mimi niko imara kama ilivyo
kuwa jana, juzi..na nitaendelea kuwa imara kwani naamini anayenilinda
bado yuko na mimi. Nayaweza haya yote kwa yeye anitiaye nguvu,” alisema
Lowassa.
Lowassa alirejea kauli yake ambayo alikwishaitoa hadharani mara kadhaa,
kuwa yeye siyo tajiri wa fedha bali wa watu na kuwashangaa wale ambao
wamekuwa wakihangaika kuwajua marafiki zake wanaomsindikiza katika
harambee za kuchangia shughuli za kimaendeleo anazozifanya katika sehemu
mbalimbali nchini.
Kabla ya Lowassa kuzungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema kuwa kuna kikundi cha wanasiasa wahuni
wanaojaribu kumkatisha tamaa Lowassa kwa maneno machafu dhidi yake.
“Kuna kikundi cha wanasiasa wahuni, wenye wivu na roho ya korosho dhidi
ya Lowassa, wanasema sema maneno ya hovyo hovyo ya kihuni, lakini sisi
tunasema usikate tamaa huo ni wivu tu, kazi unazozifanya kulitumikia
taifa hili kila mtu anaziona,” alisema Mgeja.
Kauli hiyo ya Mgeja inafuatia kauli zenye mwelekeo wa shutuma ambazo
amekuwa akielekezewa Lowassa na baadhi ya wanasiasa, kuwa anatumia fedha
chafu kuchangia shughuli za maendeleo ya kijamii.
-Mtanzania
No comments :
Post a Comment