VILIO vimeendelea kutikisa nchini Kenya, baada ya kundi la magaidi wa
kundi la Al-Shabaab kufanya mauaji ya kutisha jijini Nairobi. Wakati
vilio hivyo vikiendelea, jana Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alilihutubia
taifa na kusema wahusika wote watakamatwa na kuchukuliwa hatua
zinazostahili.
Akihutubia katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyetta
alisema vita dhidi ya ugaidi siyo ya Wakenya peke yao bali ni ya dunia
nzima, kwa kuwa magaidi yanaua watu katika maeneo mbalimbali duniani.
Alisema kwamba, Kenya haitarudi nyuma kupambana na ugaidi kwani Serikali
yake haitakubali raia wa Kenya wauawe bila sababu.
“Viongozi wote tumesimama hapa tukiomba amani na tunawahakikishia wananchi kuwa tumeweka usalama wa kutosha.
“Hakuna
anayependa kusikia ndugu yake amefariki katika shambulio la kutisha
kama lile, mimi nimepoteza jamaa zangu wawili, mpwa wangu na mchumba
wake.
“Napenda niwahahakishie Wakenya wote, kuwa wana usalama
wetu na intelijensia yetu wanafanya kazi kwa umakini, mnachotakiwa ni
kuwapa ushirikiano.
“Hatutarudi nyuma katika kupambana vita dhidi ya ugaidi na tunaomba dunia ituunge mkono katika hilo,” alisema Rais Kenyatta.
Wakati
wa hotuba hiyo, viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani walikuwapo
akiwamo Musalya Mudavadi na Raila Odinga aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa
nchi hiyo.
Viongozi hao wote, walipewa fursa ya kuzungumza ambapo walilaani tukio hilo kwa nyakati tofauti.
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Israel jana lilijitosa kusaidiana na askari wa
Kenya kuwakabili wanamgambo hao wa Somalia waliojichimbia katika jengo
la maduka ya kisasa la Westgate mjini Nairobi.
Hadi gazeti hili
linakwenda mitamboni, taarifa zilisema waliopoteza maisha walikuwa ni 69
na wengine zaidi ya 175 walikuwa wamejeruhiwa.
Katika eneo la
tukio, milio ya risasi na mizinga ilisikika wakati askari wakijaribu
kuwaua au kuwakamata washambuliaji waliokuwa wamesalia ili kumaliza
umwagaji damu uliodumu kwa saa karibu 30 katika duka hilo lililopo
Barabara ya Mwanzi huko Westlands, karibu na duka jingine maarufu la
Sarit.
“Waisrael ndio wameingia na wanawaokoa mateka na watu waliojeruhiwa,” chanzo cha habari cha jeshi la Kenya kilisema.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ilikataa kukanusha au kuthibitisha ushiriki wa jeshi lake katika operesheni hiyo.
Wapiganaji
hao wa Al-Shabaab wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda,
walidai kushiriki shambulio hilo katika jumba hilo ambalo Waisrael wana
sehemu ya hisa.
Wanamgambo hao walisema shambulio hilo ni ulipaji
kisasi ili kupinga uwepo wa jeshi la Kenya nchini Somalia ambako jeshi
la Umoja wa Afrika (AU) linapambana na makundi ya wanamgambo wa
Kiislamu.
Msemaji wa Al-Shabaab, Sheikh Ali Mohamud Rage, alidai
walikuwa wameionya Kenya, lakini ikapuuza na kuendelea uvamizi wa ardhi
yao kwa nguvu, huku wakiwaua raia wasio na hatia.
Alisema kwamba, wataendelea kufanya mashambulizi nchini Kenya hadi itakapoviondoa vikosi vyake Somalia.
“Iwapo
mnataka Kenya iwe na amani, itatokea iwapo tu vijana wenu wataondoka
katika ardhi zetu,” taarifa yake katika mtandao wa Twitter ilisema.
Hata hivyo, mtandao huo wa kijamii baadaye uliifunga akaunti yao hiyo.
Ujumbe
kutoka Twitter ulisomeka kuwa akaunti hiyo imefungiwa, ikiwa ni mara ya
tatu mwaka huu kwa kundi hilo kufukuzwa kutoka mtandao huo.
Kwa
mujibu wa Twitter, watumiaji hufungiwa kuutumia iwapo wanatumia akaunti
zao kwa malengo mabaya au kulenga shughuli zisizo halali.
Waziri
wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema watu 69
walithibitika kufariki huku Shirika la Msalaba Mwekundu likisema idadi
ya waliojeruhiwa ni takribani watu 200.
Lenku alisema kulikuwa na
wanamgambo kati ya 10 hadi 15 katika kituo hicho cha biashara.
‘Tunaamini kuna idadi ya watu isiyojulikana wasio na hatia katika jengo
na ndiyo maana operesheni hii imekuwa ngumu,” alisema.
Kwenye tukio raia wa kigeni kadhaa waliuawa akiwemo mwanadiplomasia mmoja wa Canada.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, anabiliwa na changamoto yake kuu ya kwanza ya usalama tangu achaguliwe Machi mwaka huu.
Katika
hotuba yake katika televisheni juzi, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
alisema alipoteza mmoja wa jamaa zake katika shambulio hilo.
Hata hivyo, baadaye ilifahamika dada mkubwa wa Kenyatta, Christine Wambui Pratt (61), alinusurika.
Pratt alikuwa mmoja wa wateja waliokuwapo katika kituo hicho cha biashara wakati wa shambulio hilo.
Alionekana
akikimbia akiwa amevaa kitopu cheupe, sketi ya khaki, akiwa pekupeku na
mikononi ameshika viatu vyake vyeusi na begi huku akiongozwa na mlinzi.
Pratt alipokewa na marafiki na kusindikizwa katika gari aina ya
Mercedes, iliyokuwa ikimsubiri kwenye Barabara ya Peponi. Hata hivyo
hakuwa amejeruhiwa.
Jengo hilo la maduka ya Westgate, maarufu kwa
Wakenya wa kipato cha juu na wataalamu wa kigeni lilikuwa limejaa
wateja takribani 1,000 wakati magaidi hao walipolivamia mchana wa juzi.
Wanamgambo
hao walirusha maguruneti na kuanza kumimina risasi kiholela lakini saa
chache baada ya makabiliano ya risasi, duru za usalama zilisema polisi
na jeshi walifaulu kuwazingira magaidi katika eneo moja na kufaulu
kuwaokoa mamia ya wateja na wafanyakazi wa jumba hilo.
Mashirika
ya usalama ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu yalikuwa yakihofia kuwa
kituo hicho siku moja kitalengwa na makundi yanayohusishwa na Al Qaeda
kutokana na wingi na aina ya wateja wake wanaohusisha mataifa ya
magharibi na Israel kama mwana hisa.
Shambulio hilo ni baya zaidi kutokea nchini hapa tangu Al-Qaeda walipoulipua ubalozi wa Marekani na kuua watu 200 mwaka 1998.
Shirika
la Msalaba Mwekundu la Kenya, liliomba msaada wa damu na mamlaka
ziliwahimiza wakazi wa karibu na eneo hilo kuwa waangalifu.
“Bado
tunapambana na washambuliaji na majeshi yetu yamefanikiwa kuwadhibiti
katika moja ya ghorofa,” alisema msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali Cyrus
Oguna. “Tuna matumaini kumaliza kadhia hii leo (jana),” alisema.
“Nilisikia
kelele na milio ya bunduki eneo lote, niliogopa sana, nilijaribu
kushuka ngazi na niliona mtu akikimbia kuja juu, niligeuka kurudi
nilikotoka na kujificha nyuma ya moja ya magari,” Umar Ahmed mwenye umri
wa miaka 18 alisema.
Saa chache baadaye, shambulio lilianza na
kuwashtusha watu wa rika na rangi zote ambao waliweza kuonekana
wakikimbia kutoka jumba hilo, huku wengine wakiwa wamewakumbatia watoto
wao na wengine wakitambaa kutani kuepuka kudunguliwa risasi.
“Walizungumza
lugha inayoonekana kama Kiarabu au Kisomali,” alisema mwanaume mmoja
aliyenusurika ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la Jay.
“Niliona watu wakiuawa baada ya kuulizwa waseme kitu fulani,” Jay alisema.
Baadhi
ya mashuhuda walisema wakati walipovamia, kabla ya kuanza mashambulizi
yao, wanamgambo waliwaambia Waislamu waondoke na wasio Waislamu
watalengwa na mashambulizi.
“Walikuja na kusema, “Iwapo wewe ni Muislamu, simama, tumekuja kuwaokoa,” Elijah Lamau alisema.
Alisema Waislamu waliondoka huku mikono yao ikiwa juu na kisha wanamgambo wakawapiga risasi watu wawili na kuwaua.
Watu hao wawili waliopigwa risasi na kufa inasemekana walishindwa kujibu swali kuhusiana na dini ya Kiislamu.
Naye,
Charles Karani, 41, mhandisi wa Teknolojia ya Habari alikuwa na haya ya
kusema: ‘Nilijificha ndani ya gari nikiwa na binti yangu. Niliwaona
wanaume wapatao 40 wakiwa mstalini.
“Waliulizwa nani ni Muislamu,
walioweza kuthibitisha kwa kutaja jina la mama wa Mtume waliachiwa,
lakini wale waliokosea walipigwa risasi,” alisema.
Shuhuda
mwingine, Fred Ngoga Gateretse, ambaye ni Ofisa wa Umoja wa Afrika (AU)
alisema, “Naamini, watu hawa ni walengaji wazuri sana wa shabaha kwa
sababu ukijionea jinsi wanavyoachia risasi, utajua wamefunzu mafunzo ya
kijeshi,”alisema.
Baada ya uvamizi huo, polisi wa Kenya,
wanajeshi na vikosi maalumu viliwasili na moja kwa moja kwenda katika
maeneo mbalimbali ya kituo hicho wakipita duka moja baada ya jingine.
Maofisa usalama wa kigeni mbali ya Israel, pia walikuwapo Wamarekani na Uingereza ambao walionekana wakati wote wa tukio hilo.
Mwandishi
mmoja wa Televisheni ya Shirika la Habari la Ufaransa (AFPTV), alisema
aliona watu takribani 20 wakiokolewa kutoka duka la wanasesere, baadhi
yao wakiwa watoto waliobebewa kwenye machela.
Kenneth Kerich,
ambaye alikuwa akifanya ununuzi wakati shambulio likitokea, alieleza
hali halisi ilivyokuwa ya kutisha na kushtusha mno.
“Ghafla
nilisikia milio ya bunduki na niliona kila mtu akikimbia huku na kule na
hivyo tulilala chini. Niliona watu wawili wakiwa sakafuni wakivuja
damu, nadhani walipigwa risasi,” alisema.
“Wanamgambo walijaribu
kulenga kichwa change, lakini walinikosa, niliona watu wapatao 50
wakipigwa risasi,” mmoja wa wafanyakazi katika kituo hicho, Sudjar Singh
aliiambia AFP.
Miongoni mwa waliokufa ni mshairi maarufu wa
Ghana na mwakilishi wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Awoonor
(78), huku mwanae akijeruhiwa, kwa mujibu wa maofisa wa Ghana.
Hii si mara ya kwanza kwa maslahi ya Israeli nchini Kenya kushambuliwa.
Novemba
2002, kulikuwa na mashambulizi mawili mjini Mombasa, la kwanza likiwa
la kombora lililolenga ndege ya kukodi ya Israeli wakati ikiruka kwenye
uwanja wa ndege wa mji huo wa bandari, lakini liliikosa.
La pili
lilihusisha gari lililokuwa limesheheni mabomu ambalo liliparamia Hoteli
Paradise, hoteli pekee inayomilikiwa na Israel mjini Mombasa, huku
watalii wa Israeli waliowasili mahali hapo muda mfupi, wakiwa eneo la
mapokezi ya hoteli hiyo.
Wakenya 10 na Waisrael watatu walikufa katika shambulio hilo.
Mkuu
wa Sera ya Kigeni ya Umoja wa Ulaya (EU), Catherine Ashton, alieleza
kushtushwa na shambulio hilo la kinyama dhidi ya raia wasio na hatia
mjini Nairobi.
Ufaransa imethibnitisha raia wake wawili ni miongoni mwa waliokufa katika kile ilichokiita shambulio la uoga.
Waziri
Mkuu wa Canada, Stephen Harper, alisema raia wawili wa Canada, akiwamo
mwanadiplomasia, walikuwa miongoni mwa waliokufa, huku Shirika la Habari
la China (Xinhua) likisema mwanamke raia wa taifa hilo alikufa na mtoto
wake kujeruhiwa.
Raia wawili wa India na mmoja wa Korea Kusini pia ni miongoni mwa waliofariki.
Marekani ilisema raia wake ni miongoni mwa walioripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Ikulu
ya Marekani (White House) ililitaja tukio hilo kuwa la kikatili. Aidha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alisema nchi yake imetoa
msaada kwa Serikali ya Kenya ili kusaidia kuikabili hali hiyo.
Naye
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, alisema wana
uhakika raia wa Uingereza walikuwa wakishikiliwa mateka na hivyo
wanapaswa kujiandaa kwa habari zozote mbaya.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, alikuwa akifuatilia shambulizi hilo kwa karibu huku akililaani vikali.
-Mtanzania.
No comments :
Post a Comment