SHULE ya Sekondari ya Ilboru, jijini Arusha imefungwa kwa muda usiojulikana kuanzia leo baada ya kuwepo hofu ya kuchomwa moto.
Uchunguzi
wa madai ya shule hiyo kuchomwa moto, unaendelea kufanywa huku
ikielezwa kwamba wanafunzi wanne wanahojiwa na polisi wilayani Arumeru
wasaidie kubaini ukweli juu ya madai hayo.
Wanafunzi wengine 10 inadaiwa wamepewa barua za kusimamishwa shule kwa siku kadhaa wakihusishwa na suala hilo.
Tangazo
la kufunga shule hiyo lilitolewa ghafla leo asubuhi na Mkuu wa Shule,
Julius Shila baada ya kushauriana na bodi yake, huku polisi wa kawaida
wakifanya doria kudhibiti vurugu zozote ambazo zingeweza kutokea.
Ingawa
Mkuu wa Shule, Shila hakutaka kuzungumzia suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu
wa Mkoa, Sifael Mollel, alisema uchunguzi wa madai hayo unaendelea
katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wamepewa likizo.
Alisema
kuwepo kwa hofu hiyo na wasiwasi wa kuzuka vurugu ndiko kulikosababisha
shule ifungwe kwa muda licha ya kwamba walikuwa hawajamaliza mitihani.
“Uongozi
umeamua wanafunzi warudishwe nyumbani kutokana na hofu ya kuchomwa moto
shule, wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani kabla ya kuanza likizo
fupi lakini uwepo tishio hilo na kuzuka kwa vurugu, ilionekana ni vema
ikafungwa,” amesema.
Alisema
kwa kawaida likizo fupi ni ya siku 10 lakini kwa tukio hili wanafunzi
hao wamepewa maelekezo ya kwenda kuonana na wakuu wa wilaya zao kwa
udahili kabla ya kurejea tena shuleni.
Akizungumzia
vitisho vya moto, alisema wanafunzi hao waliwasilisha barua ofisini
kwake wakitoa madai kuwa baadhi ya walimu walikuwa wanataka kuchoma moto
shule hiyo.
Alisema polisi walienda kufanya uchunguzi Ijumaa ambapo walinusa harufu ya petroli iliyokuwa imemwagwa jirani na bweni.
Hata
hivyo Kaimu Ofisa Elimu huyo hakutawataja wanafunzi ambao wanahojiwa na
polisi wala wanafunzi 10 ambao wamesimamishwa kwa siku 21.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, alikiri polisi kuwepo shuleni hapo
wakati tangazo la kufungwa shule likitolewa akasema hiyo ilikuwa ni kwa
sababu ya kuimarisha usalama.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wanafunzi wote watatakiwa kurejea shuleni hapo baada ya kudahiliwa na wakuu wa wilaya zao.
No comments :
Post a Comment