- Viza hizo za kipaumbele zinatazamiwa kutolewa katika makundi mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara, wanafunzi na wale wanaokwenda kwa matembezi ya kawaida.
Ili
kuimarisha biashara, Ubalozi wa Uingereza nchini umesema, kuanzia sasa
Watanzania wanaotaka huduma za viza kwa ajili ya kwenda nchini humo
wanaweza kupata huduma hiyo katika kipindi cha muda mfupi kutokana na
kuanzishwa kwa kile kinachoitwa ‘viza za kipaumbele’.
Huduma hiyo ambayo pia imeanza kutumika katika
nchi nyingine za Uganda na Kenya inaelezwa kuwa ni moja ya mkakati wa
Serikali ya Uingereza kuongeza kasi ya ushirikiano na uwekezaji nchini.
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema
uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili umeimarika zaidi katika
miaka ya hivi karibuni hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya kutasaidia
kuharakisha kufikia malengo ya kibiashara kwa pande zote.
“Huduma hii ya kipaumbele itahakikisha maombi ya
viza yanafanyiwa kazi ndani ya siku tano na mwombaji atatakiwa kulipia
kiasi cha Sh250,000,” alisema Balozi Melrose.
Hata hivyo, alifafanua kuwa, pamoja na kuanzishwa
kwa huduma hiyo mpya, zoezi la utoaji viza litaendelea kufanywa kwa
kufuata sheria za kawaida za uhamiaji.
Viza hizo za kipaumbele zinatazamiwa kutolewa
katika makundi mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara, wanafunzi na wale
wanaokwenda kwa matembezi ya kawaida.
Alisisitiza kuwa viza za kipaumbele zina lengo la
kufanya mchakato wa maombi kuwa wa kasi zaidi hasa kwa wafanyabiashara
pamoja na wengine ambao watahitaji kufanya maombi ndani ya muda mfupi.
“Tunafanya hivi kutokana na maombi ya wengi, pia
kutokana na kukua kwa uhusiano wa kibiashara ili kuleta maendeleo na
ajira kwa Watanzania na Waingereza,” alisema Balozi Melrose.
Kuhusu utoaji viza kupitia ubalozi wake Nairobi,
Kenya, Balozi Melrose alisema “Tunafanya hivyo ili kuwa na ufanisi mzuri
wa kazi na hakuna upendeleo wowote.”
No comments :
Post a Comment