Bi Kidude alifariki dunia Aprili 17, mwaka huu baada ya kulazwa kwa muda mrefu akisumbuliwa na maradhi ya Kisukari na uvimbe kwenye kongosho.
MJUKUU WA BI KIDUDE
Mara baada ya kutokea kwa msiba huo mkubwa, mjukuu wa marehemu Bi Kidude aliyekuwa akimuuguza, Omary Abdallah aliliambia Ijumaa: “Kwa ufupi Bi Kidude alilazwa kipindi kirefu na baadaye akatolewa.”
JITIHADA ZA KUOKOA MAISHA
“Baadaye alianza tena kuumwa tukampeleka hospitalini. Tukawa tunampeleka kwenda na kurudi. Siku tatu nyuma (kabla ya kifo) alizidiwa tena zaidi tukampelekea kwenye hospitali moja inaitwa Kaeeni (Zanzibar) kwa ajili ya matibabu zaidi, dripu na vitu vingine.
MUNGU ACHUKUA ROHO YAKE
“Baada ya siku ya tatu, Mungu akachukua roho yake. Kiukweli aliteseka sana kwa muda mrefu.”
Ijumaa: Kwani amefariki wapi?
Omary: Amefariki nyumbani kwa mtoto wa kaka yake huku Bububu (Zanzibar).
Ijumaa: Madaktari walisema tatizo lililosababisha kifo hasa ni nini?
Omary: Unajua alianza kuumwa muda mrefu, sema tu watu walikuja kujua baadaye. Alikuwa akiteswa na Kisukari na uvimbe kwenye kongosho.
MATESO
Bi Kidude alianza kuuga muda mrefu tangu mwaka 2011.
Mara kadhaa magazeti ya Global Publishers yalifunga safari hadi Zanzibar kwenda kumjulia hali na kuiripoti kwa mashabiki wake.
ALETWA BARA
Kuna kipindi hali ilikuwa mbaya hadi akaletwa Tanzania Bara katika Hospitali ya Hindu Mandal, Dar ambapo viongozi mbalimbali wa serikali walifika kumjulia hali.
Hata hivyo, alipopata ahueni, alirejeshwa nyumbani Zanzibar na kuendelea na matibabu huko.
MBALI NA MARADHI
Katika mahojiano na watu mbalimbali, ukiondoa maradhi, tangu umri wake ulipovuka miaka 90 ndipo matatizo ya uzee yalipoanza hadi alipokutwa na umauti zaidi ya miaka 10 baadaye.
‘AFA’ MARA 13
Katika kuumwa kwake, Bi Kidude alizushiwa kifo takriban mara 13 na kusababisha taharuki hadi Mungu alipomchukua kiukweli.
Kufuatia hali yake ya kiafya, mwanzoni mwa mwaka huu alithibitishwa kutoshiriki katika Tamasha la Zanzibar Films Festival (ZIFF) na kuaga kwamba hatashiriki tena.
HISTORIA
Bi Kidude alikuwa msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarab.
Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki kutoka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umejikita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
KUZALIWA
Bi Kidude, alizaliwa katika Kijiji cha Mferejimarigo, Zanzibar katika familia ya watoto saba.
Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa Zanzibar.
UTATA WA UMRI
Bi Kidude hakujua tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alichojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia (aina fedha) ikitumika kama fedha na vilevile alikuwa na uhakika kuwa alizaliwa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1917-1919.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 104 hadi sasa.
AANZA MUZIKI
Bi Kidude alianza muziki alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo, Sitti Binti Saad.
Wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumuona Sitti.
Kwa kuwa Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu, basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba.
Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri katika uimbaji wa muziki wa mwambao.
Alipokuwa na umri wa miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa.
NDOA
Bi Kidude alipokuwa kigori wa kutosha kuolewa, aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na...
manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hakutaka kuolewa tena hivyo aliamua kukimbilia Kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930.
ANG’ARA MISRI
Huku Misri aling’ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma.
Ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.
Bi Kidude hakutegemea kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara wa ‘wanja’ na ‘hina’ ambavyo alivitengeneza yeye mwenyewe.
Pia alikuwa mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo alikuwa mwalimu mzuri sana wa ‘unyago’.
Enzi za uhai wake, Bi Kidude alianzisha chuo chake mwenyewe cha unyago na alichokuwa akijivunia, wanafunzi wake wote hawakupata talaka katika ndoa zao.
SHUJAA
Watu walisema ‘utu uzima dawa’, Bi Kidude alikuwa mwanamke shujaa na mwenye upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za Kiarabu ambapo mwanamke alitakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, aliliona hilo katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake.
Bi Kidude alikuwa mnywaji wa pombe na nvutaji wa sigara, jambo ambalo halikuwa kawaida kwa wanawake wa Zanzibar.
ZIARA ZA KIMUZIKI
Katika kazi zake za muziki, Bi Kidude alifanya ziara nchi nyingi zikiwemo Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
TUZO
Bi Kidude alijizolea tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 ambayo ni tuzo ya maisha.
KUTOKA KWA JK
Mwaka 2012 alipata tuzo ya mwanamke ya WOMAX kabla ya mwaka huu kuchukua ile ya heshima kwa mwanamuzki aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania, tangu uhuru aliyokabidhiwa na Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
NYIMBO
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa Jang’ombe, Kijiti, Yalaiti na nyingine kibao hasa zile alizoshirikishwa na wasanii kama AT, Off-Side Trick, Fid Q na wengineo.
ELIMU
Bi Kidude hakupata elimu nyingine zaidi ya ile ya Kurani.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amen!
No comments :
Post a Comment